NA JOHN BUKUKU, SINGIDA
Mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, amepongeza watumishi wa umma kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo sambamba na CCM kuendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi hiyo ili kuhakikisha inalingana na thamani ya fedha zinazotolewa na serikali.
Amesema, chama hicho kimekuwa mstari wa mbele kuikagua miradi mbalimbali ya maendeleo na pale inapobainika kuwa haijakidhi vigezo, kimeikataa ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na maendeleo yanayostahili.
Dkt. Samia aliyasema hayo leo alipohutubia maelfu ya wananchi wa Mkoa wa Singida waliojitokeza kwa wingi kumsikiliza wakati akiendelea na kampeni za kuomba ridhaa ya kuongoza Tanzania kwa kipindi cha mwaka 2025–2030.
Katika mkutano huo uliohudhuriwa na utitiri wa wananchi waliokuwa na bashasha na tabasamu, Dkt. Samia alisema kuwa serikali ya awamu yake itahakikisha Mkoa wa Singida unapata miradi mikubwa ya kiuchumi ikiwemo ujenzi wa Soko Kuu la Kimataifa la Vitunguu pamoja na Soko la Machinga Complex, ili kuchochea shughuli za kibiashara na kuongeza kipato cha wananchi.
Amefafanua kuwa ndani ya kipindi cha miaka minne iliyopita, Mkoa wa Singida umepokea zaidi ya shilingi trilioni 1.7 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa hospitali 4, vituo vya afya 22 na zahanati 63.
Aidha, amesema serikali inaendelea kufanya jitihada za kutafuta masoko ya mazao ya wakulima ili kuhakikisha wanapata bei nzuri, huku akiahidi kuendeleza mageuzi katika sekta ya kilimo kwa maendeleo endelevu ya wananchi.
Kwa upande wao baadhi ya wagombea ubunge kupitia CCM mkoani Singida akiwemo Dkt. Mwigulu Nchemba (Iramba Magharibi) na Elbarick Kingu (Ikungi Magharibi) walimpongeza Dkt. Samia kwa kazi kubwa alizofanikisha ndani ya kipindi cha miaka minne.
Naye Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM, Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, alisema chama hicho kimekuwa na jukumu kubwa la kuisimamia serikali kwa kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi, huku akisisitiza kuwa Dkt. Samia ni mgombea mtulivu, makini na jasiri ambaye ameendelea kulinda misingi ya chama na kuwaletea maendeleo wananchi.