KATI ya wachezaji 11 wapya waliotua Yanga kwa ajili ya msimu wa 2025-2026, kiungo mshambuliaji Celestine Ecua mapema tu ameonekana kuwashtua mabosi wa timu hiyo.
Ecua ambaye hivi karibuni akiwa na kikosi cha timu ya taifa ya Chad alifunga bao dhidi ya Ghana kisha kuwapa jeuri kubwa mashabiki wa Yanga, ameshtua kutokana na uamuzi alioufanya akiwa kambini.
Taarifa kutoka Yanga, zinabainisha, Ecua amewapigia simu mabosi wa timu hiyo akiwaambia anataka kuwahi Dar kutoka kambi ya timu ya taifa ili apate maandalizi kabambe kuelekea Tamasha la Wiki ya Mwananchi na mchezo wa Ngao ya Jamii.
Ecua amewaambia mabosi wa Yanga, kama Chad itachelewa kumtumia tiketi ya ndege basi, klabu yake ikae tayari kumtafutia haraka kwani anataka kuwahi nchini.
“Ecua amepiga simu anasema amemwomba meneja wa timu ya taifa lake ahakikishe anaondoka Madagascar mara baada ya mchezo kumalizika, wakamwambia sawa,” kilisema chanzo hicho.
“Licha ya jibu hilo, Ecua akaona atupigie ili tujiandae kama Chad wakichelewa kumtengenezea tiketi hiyo, sisi huku tumfanyie wepesi kumpa tiketi ya kumtoa kule haraka ili awahi Tamasha la Wiki ya Mwananchi.
“Kiukweli ametushtua sana, ameonyesha ni mchezaji ambaye anataka mambo makubwa kwa ajili ya mashabiki wa klabu yake.”
Wakati hayo yakiendelea, katika mchezo dhidi ya Madagascar uliochezwa Septemba 8, 2025 na Chad kupoteza kwa mabao 3-1, Ecua hakuwa sehemu ya kikosi hicho hata benchi.
Hilo limedhihirisha nyota huyo ameondoka mapema zaidi kwani mchezo huo haukuwa na umuhimu sana kufuatia Chad kutokuwa na nafasi ya kufuzu ikiwa inaburuza mkia wa Kundi I ikikusanya pointi moja katika michezo sita iliyocheza.
Ikumbukwe kuwa, Septemba 12 mwaka huu, Yanga itakuwa na Tamasha la Wiki ya Mwananchi ikiwa ni msimu wa saba tangu kuanza kwake mwaka 2019 ambapo mbali na burudani mbalimbali, pia kutakuwa na utambulisho wa kikosi cha timu hiyo kwa msimu wa 2025-2026 na mchezo wa kirafiki dhidi ya Bandari ya Kenya.
Wakati wa utambulisho wa kikosi, wengi watataka kuwaona nyota wapya waliotua kikosini hapo ambao ni Frank Assinki, Moussa Balla Conte, Offen Chikola, Abdulnassir Mohamed Abdallah ‘Casemiro’, Abubakar Nizar Othuman ‘Ninju’, Andy Boyeli, Lassine Kouma, Mohamed Doumbia, Mohamed Hussein, Edmund John na Celestin Ecua.
Kocha Mfaransa atoa neno
Kitendo cha Ecua kupiga bao kwenye mchezo wake wa kwanza akiwa na Chad baada ya kuamua kulitumikia taifa hilo tofauti na Ivory Coast alipozaliwa, imemfanya kocha wake wa zamani Jullie Chalier kusema kuna mambo mengi zaidi nyota huyo atayaonyesha Yanga.
Ecua akiwa na timu ya taifa ya Chad ikiwa nyumbani katika mchezo wa kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2026 uliochezwa Septemba 4, 2025, alifunga bao la kusawazisha dakika ya 89 kwa shuti kali baada ya kuupita ukuta wa wapinzani. Hata hivyo, Chad iliyopo Kundi I, haina nafasi ya kufuzu ikiburuza mkia na pointi moja baada ya kucheza mechi sita.
Akizungumzia bao hilo, Chevalier ambaye alifanya kazi na Ecua akiwa ASEC Mimosas msimu uliopita, alisema mabao ya aina hiyo ni kawaida kwa Ecua kwani ana ujuzi nayo sana.
Raia huyo wa Ufaransa alisema, kama timu pinzani hazijajipanga sawasawa, basi muda ndiyo huu zijiandae na mambo kama hayo aliyofanya Ecua mbele ya Ghana kwani vinginevyo atasumbua.
“Watu wameshangilia bao lile, basi waambie wajiandae kuona mabao zaidi ya namna ile, yule ndio Ecua, huko litakuwa bao jipya kwa kuwa hajawahi kucheza, lakini watayaona sana mabao kama yale.
“Akiwa hapa ASEC amefunga sana mabao ya namna ile, huyu ni mchezaji ambaye anapambana sana uwanjani, siyo rahisi kukata tamaa, waambie timu atakazokutana nazo hapo Tanzania zijiandae kukutana na mambo ya namna hiyo,” alisema Mfaransa huyo.
Chevalier aliongeza: “Ecua ana mbinu nyingi za kuwapunguza mabeki wa timu pinzani akiwa na kasi na akiwa na ubora wa kupiga mashuti makali.
“Bila shaka ataonyesha mambo makubwa zaidi kwa kuwa ni mchezaji mwenye kiu ya kutaka kufanya mambo makubwa akiwa uwanjani.
“Akiwa hapa alikuwa anatusaidia sana kuziadhibu zile timu ambazo zilikuwa zinapenda kucheza nyuma ya mpira kwa kujilinda zaidi, tulikuwa tunampa kazi ya kuwapangua mabeki.
“Kitu hatari zaidi ni mjuzi wa kufunga, pia muda mwingi uwanjani anapenda kufanya makubwa, anapambana sana akiwa kwenye timu yake, ukiliangalia lile bao alilofunga dhidi ya Ghana alikuwa anahangaika muda wote.”
The post BAADA YA KUIFUNGA GHANA JUZI…MSHAMBULIAJI MPYA AISHTUA YANGA….MABOSI WAKUNA KICHWA appeared first on Soka La Bongo.