PRAIA: TIMU ya taifa ya Visiwa vya Cape Verde inaweza kuwa nchi ya pili kwa udogo duniani kuwahi kufuzu kwa Kombe la Dunia baada ya kupiga hatua muhimu kulitimiza hilo baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Cameroon.
Ushindi huo wa 1-0 wa Cape Verde nyumbani dhidi ya Cameroon umewaweka pointi nne kwenye msimamo wa Kundi D mbele ya Cameroon maarufu kama ‘Indomitable Lions’ na hatma yao iko mikononi mwao wenyewe ikiwa watashinda mechi mbili za kufuzu mwezi ujao.
Visiwa hivyo vya Afrika Magharibi, vyenye wakazi zaidi ya 600,000, vilipata ushindi huo katika uwanja wao wa nyumbani wa Estádio Nacional de Cabo Verde mjini Praia kwa bao la dakika ya 54 kutoka kwa mshambuliaji Dailon Livramento, ambaye alimpokonya mpira Carlos Baleba mpira na kumuacha kipa Andre Onana asiwe na la kufanya.
Cape Verde inahitaji pointi tatu pekee kutoka kwenye mechi zao mbili za kufuzu mwezi ujao ugenini dhidi ya Libya na nyumbani dhidi ya Eswatini ili kuandika Historia ya kushiriki Kombe la Dunia kwa mara ya Kwanza.
Iceland, yenye watu takriban 350,000, ndio nchi ndogo zaidi kuwahi kushiriki fainali za kombe la Dunia zilizofanyika mwaka Urusi mwaka 2018.
The post Cape verde kuandika Historia kombe la Dunia? first appeared on SpotiLEO.