Kwamba siku moja Clatous Chama angeenda kucheza soka lake Singida Black Stars ni jambo halikufirika kwa wengi. Binafsi nililifikiria. Nina sababu zake. Tangu wakati ule akiwa Simba niliwahi kumuona Chama katika mawazo akicheza timu nyingine nje ya Simba na Yanga katika ardhi ya Tanzania.
Sababu ni rahisi tu kwamba Tanzania ni nchi tamu kwa wachezaji na makocha. Hasa ambao wamekaa hapa kwa kipindi fulani. Hatimaye Chama naye ametua Singida Black Stars. Haikuwa safari rahisi sana, lakini hatimaye amefika.
Utawala wake Simba ulikuwa mkubwa. Kinachoshangaza ni kitu kimoja tu namna maisha yalivyoenda kasi zaidi kwake katika klabu yake nyingine ya Yanga. Ndani ya miezi 12 tu kila kitu kimeenda hovyo. Chama alikwenda Yanga akiwa keki ya moto. Asubuhi ile ambayo mashabiki wa Yanga waliamka na kuona mtandao wa klabu yao ukiwa umemposti Chama kuwa mchezaji mpya, makundi ya mashabiki wa Yanga walianza kutembea na picha zake na kubandika katika kuta mbalimbali jijini Dar es salaam.
Kilichofuta baada ya hapo ni historia ambayo nadhani hata Chama mwenyewe hatapenda kuikumbuka sana. Miezi 12 ya ovyo kwa upande wake ingawa iliendelea kuwa miezi 12 mizuri kwa Yanga. Yeye hakuendelea kuwa na thamani ileile. Muda mwingi alijikuta katika benchi.
Mwisho wa msimu Yanga hawakuomuongezea mkataba Chama. Kule upande wa watani hisia zilikuwa wazi. Fununu za kumrudisha hazikuwepo. Watu walikuwa wanadai kwamba Chama alikuwa anawahujumu kwa Yanga wakati ule akiwa na jezi zao nyekundu na nyeupe. Na kitendo cha yeye kwenda Yanga kilikuwa kama ni uthibitisho kwamba kweli alikuwa anawahujumu. Ndugu wengine wa Jiji ambao wana ukwasi mkubwa Azam nao wakafuata kwamba kama Yanga imemuona mchezaji hatoshi kwao kiasi cha kuamua kuachana naye kwanini wao wamchukue? Azam wakaona bora wakomae na Fei Toto wao kuliko kushughulika na habari za Chama. Mwishowe kabisa Chama akajikuta anaangukia Singida Black Stars.. Itaendelea
— Legend Edo Kumwembe. [Hisia Zangu]