LEVERKUSEN: KOCHA wa mpya wa Bayer Leverkusen Kasper Hjulmand amesema kikosi chake kina ubora wa kutosha kufanya vyema msimu huu licha ya kufanyiwa marekebisho madogo kwenye dirisha la usajili la majira ya kiangazi na mwanzo mbaya wa msimu huu wa Bundesliga.
Kocha huyo wa zamani wa Denmark ametua Leverkusen Jumatatu baada ya Mabingwa hao wa zamani wa Bundesliga kumtimua meneja wa zamani wa Manchester United Erik Ten Hag kufuatia mwanzo mbaya kikosini hapo.
Hjulmand ana kazi ngumu ya kuiimarisha Leverkusen ikiwa imeshindwa kupata ushindi wowote kwenye Ligi hadi sasa huku Eintracht Frankfurt walio kwenye kiwango kizuri wakibisha Hodi Bayer Arena Ijumaa hii.

“Ni changamoto kubwa kwa sababu kwenye soka unahitaji michakato mizuri kuwa bora, Hubonyezi kitufe tu mambo yakawa. Lazima ufanye kazi kila siku na kuunda kilicho bora”
“Kuna ‘quality’ kubwa kikosini. Tunahitaji nguvu kidogo tu tuwake. Mapema tu tutakuwa wakali, tutakuwa timu tishio. Hatujui ni lini. Hadi wakati huo tutakuwa na dakika nzuri, na mbaya.” – Hjulmand aliuambia mkutano na waandishi wa habari.
Leverkusen walipoteza mechi yao ya ufunguzi wa ligi kwa mabao 2-1 wakiwa nyumbani dhidi ya Hoffenheim kabla ya kutoka sare ya 3-3 na Werder Bremen yenye wachezaji 10, na kusababisha Ten Hag kufutwa kazi.
The post Kocha Leverkusen atamba kukiwasha Bundesliga first appeared on SpotiLEO.






