MANCHESTER: MABINGWA wa zamani wa EPL Manchester City wamethibitisha rasmi kuwa mshambuliaji wao raia Misri Omar Marmoush ataukosa mchezo wa wikiendi hii wa Manchester derby baada kupata jeraha la goti alipokuwa akiitumikia timu yake ya taifa katika mechi ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Burkina Faso usiku wa Jumanne.
Marmoush, ambaye alijiunga na Manchester City kutoka Eintracht Frankfurt mwezi Januari mwaka huu, aliumia mapema kwenye mchezo huo na nafasi yake kuchukuliwa na Osama Faisal mnamo dakika ya10 ya mchezo.
Baada ya mawasiliano na Malaka za soka za Misri, Man City imethibitisha kuwa jeraha alilopata halitamruhusu mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 26 kuwa sehemu ya kikosi kitakachoivaa United jumapili
“Matokeo ya uchunguzi wa awali uliofanywa nchini Misri yanaonesha kuwa hatakuwepo kwenye mechi ya Manchester derby Jumapili, na sasa atarejea jijini Manchester kwa tathmini zaidi na kuanza matibabu. Tunamtakia Omar ahueni ya haraka” – imesema taarifa ya Manchester City
Marmoush ameanza katika kikosi cha kwanza cha Pep Guardiola kwenye mechi mbili kati ya tatu zilizopita na alitumika kama mchezaji wa akiba kwenye mechi ya ufunguzi wa msimu dhidi ya Wolverhampton.
The post Marmoush kuikosa United Jumapili first appeared on SpotiLEO.