DAR ES SALAAM: MSANII nyota kutoka Kenya, Benson Mutua maarufu kama Bensoul, amefichua kuwa alishiriki katika kuandika wimbo wa Katam wa Diamond Platnumz, akidai suala la wasanii kuandikiana nyimbo ni jambo la kawaida katika muziki.
Bensoul ambaye amewahi kung’arisha mashabiki kupitia nyimbo kama Lucy, Forget You, Nairobi, Favourite Song, Medicine na Extra Pressure, alianza rasmi safari yake ya muziki mwaka 2019 chini ya lebo ya Sol Generation Records ya kundi la Sauti Sol.
Bensoul amesema:“Ni ngumu sana mtu kama Bien kusema wimbo fulani ni wake.Ni vile sisi ni ndugu na nyimbo ambazo tumeandika pamoja ni nyingi.
Watu hawajui bado kuwa wimbo wa Katam wa Diamond nimeshiriki kuandika. Diamond alituma biti pekee yake, Bien akaja kuniambia tumefanyaje, nikamwambia tusikilize tuandike mistari. Mistari ya vesi ya pili tuliandika sisi kisha tukamrudishia, na Diamond naye akaongeza yake. Kwa hiyo mimi ni mmoja wa walioandika ule wimbo.”
Wimbo wa Katam ulitolewa miezi miwili iliyopita na Diamond Platnumz akimshirikisha Bien, mmoja wa wanamuziki wa zamani wa kundi la Sauti Sol.
Swali linalobaki kwa mashabiki ni je, ni sawa msanii kuandikiwa wimbo au kila mmoja aandike wake binafsi?
The post Siri ya ‘katam’ yafichuka first appeared on SpotiLEO.








