BELGRADE: BEKI wa Tottenham Hotspur, Djed Spence ameweka historia ya kuwa Muislamu wa kwanza kuichezea timu ya taifa ya England alipotokea benchi katika mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Serbia mjini Belgrade Jumanne
Spence, mwenye umri wa miaka 25, alichukua nafasi ya beki wa Chelsea Reece James mnamo dakika ya 69 ya ushindi wao 5-0 dhidi ya Serbia katika mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia la mwakani nchini Marekani, Canada na Mexico.
“Ilikuwa ‘surprise’ kwangu kwa sababu sikujua mimi ni wa kwanza, ni jambo la baraka. Ni vizuri kuweka historia na kuwa hamasa kwa vijana wengine kote Duniani kwamba inawezekana. Wanaweza kufanya kile ninachofanya.” – Spence mzaliwa wa London alisema.
Kuonekana kwa Spence ndani ya ‘uzi’ wa timu hiyo ya kwa mara ya kwanza kunachukuliwa kama tukio muhimu kwa Waislamu kote nchini England kufuatia Kundi hilo kuwa na uwakilishi mdogo katika soka la kulipwa nchini humo, licha ya Waislamu kuwa ni asilimia 6 ya watu wote.
Spence alianza soka lake na Middlesbrough kabla ya kujiunga na Tottenham mwaka 2022 ambako alikuwa na mwanzo mgumu klabuni hapo akitolewa kwa mkopo mara 3, kabla ya ‘kupata moto’ na kupata nafasi kwenye mchezo wa fainali wa Europa League msimu uliopita.
The post Spence aweka historia England first appeared on SpotiLEO.