BURUNDI: NAHODHA wa Timu ya Taifa ya soka kwa watu wenye ulemavu, Tembo Warriors, Bashra Alombile, amekiri kuwa matokeo ya mechi yao ya jana dhidi ya Kenya hayakuridhisha.
Katika ufunguzi wa mashindano hayo ya Afrika Mashariki na Kati ya Soka kwa Watu Wenye Ulemavu (CECAAF) timu yake ilifungwa mabao 2-0, lakini Bashra amesema kuwa wachezaji wake wanachukua kipigo hicho kama funzo muhimu.
“Matokeo kwetu hatujapata ya kuridhisha; haukuwa mpango wetu. Niseme mpira umekuwa na matokeo ya kikatili na sisi tumeyapokea, imekuwa ni funzo. Bado kuna mechi nyingine tunahitaji kujipanga vizuri kupata matokeo mazuri,” alisema Bashra.
Timu ya Tembo Warriors iliyoko Kundi B inatarajia kukutana na Uganda katika mchezo unaofuata.
Bashra amesema ana matumaini benchi la ufundi litarekebisha makosa waliyofanya na kupata ushindi katika mchezo huo ujao.
Tembo Warriors ndio watetezi wa kombe hilo walilolitwaa mwaka jana. Michuano hiyo inatarajiwa kumalizika Septemba 14, mwaka huu.
The post Tembo Warriors yapata funzo Kenya first appeared on SpotiLEO.