Rushine De Reuck ameanza kuandika historia mpya ndani ya kikosi cha Simba SC kwa namna ya kipekee kabisa. Ni vigumu kumpuuza beki huyu wa kati ambaye ameonesha kiwango cha juu sana ndani ya muda mfupi tangu ajiunge na timu hiyo. Katika ulimwengu wa soka, mchezaji mzuri hachukui muda mrefu kuonesha uwezo wake, na kwa Rushine, mechi moja tu ya Simba Day dhidi ya Gor Mahia imetosha kumpa heshima na imani ya mashabiki wengi.
Kwa wanaofuatilia soka kwa undani, beki mzuri si yule anayekimbia sana au kupiga kelele, bali anayesoma mchezo, anayeweka nafasi vizuri, na anayechukua maamuzi sahihi kwa wakati sahihi. Rushine ameonesha haya yote. Katika kila hali, anasubiri mshambuliaji afanye kosa au movement ya kwanza, kisha yeye huingilia kati kwa ustadi mkubwa kuondoa mpira bila kumvunja mchezaji. Hii ni sifa adimu inayopatikana kwa mabeki waliokomaa kimchezo na kifikra.
Mbali na uwezo wake wa kuingilia kati mashambulizi kwa kutumia standing tackle na sliding tackle kwa utulivu, anajua kutumia mwili wake kwa ustadi mkubwa bila kufanya faulo. Ni aina ya beki ambaye haogopi presha, anacheza kwa akili na anajiamini bila haraka zisizo na maana. Wachezaji wa aina hii huongeza thamani ya timu si tu kwa ulinzi imara bali pia kwa utulivu wanaoleta kwa timu nzima.
Changamoto pekee ambayo imekuwa ikitajwa kuhusu Rushine ni historia yake ya majeraha, jambo ambalo linaweza kuwa tishio kwa msimu mrefu. Hata hivyo, iwapo ataendelea kuwa fiti na kuepuka majeraha, basi Simba wamepata hazina kubwa. Katika mechi ya Simba Day, alionesha ni kwa nini alikuwa chaguo la kwanza katika timu aliyotoka, na sasa yuko kwenye mwelekeo wa kuwa miongoni mwa mabeki bora zaidi waliowahi kucheza Tanzania.
Ujio wake unaipa Simba matumaini mapya katika ngome ya ulinzi, haswa katika mashindano ya kimataifa ambayo mara nyingi huhitaji mabeki wenye uzoefu, akili na uthabiti. Rushine De Reuck anaonekana si tu kuongeza ushindani katika safu ya ulinzi, bali pia kuwapa changamoto wachezaji wa ndani kujiinua zaidi. Kwa sasa, hana cha kuthibitisha tena ameanza kutimiza ahadi ya kuwa “top defender” halisi.









