Katika kuelekea mashindano makubwa yanayokaribia, Simba SC imeonesha dhamira ya kujenga timu imara, lakini bado kuna mambo kadhaa yanayohitaji kufanyiwa kazi kwa haraka. Mechi dhidi ya Gor Mahia imekuja wakati sahihi – si tu kama kipimo cha maandalizi, bali pia kama nafasi ya kujifunza. Gor Mahia hawakuja kutalii, walikuja kucheza mpira, hali ambayo imewasaidia Simba kuona maeneo yanayohitaji maboresho.
Kwanza, ni wazi kuwa wachezaji wengi wapya wameingia kwenye kikosi. Hili lina faida lakini pia changamoto zake. Pia, wapo wachezaji waliotumika sana msimu uliopita na wanahitaji muda wa kupumzika. Wakati huo huo, wapo waliokuwa nje kwa muda mrefu na sasa wanahitaji dakika za kucheza ili warudi kwenye kiwango chao. Hii inahitaji usawa mkubwa wa kiufundi kutoka kwa benchi la ufundi.
Fadlu David, kocha mkuu wa Simba, ana kazi ya haraka ya kuhakikisha uimara wa kimwili wa wachezaji unarejea. Baadhi yao bado hawapo kwenye kiwango kinachohitajika, hasa kwa ajili ya mashindano yanayokuja. Pia, lazima atafute ‘combinations’ sahihi hasa kwenye safu ya ulinzi na kiungo. Wachezaji wanaopangwa kwa pamoja lazima wawe na sifa zinazokamilishana badala ya kudhoofishana.
Bila mpira, Simba walionekana na changamoto za kimbinu. Mfano mzuri ni pale Ahoua na Maema walipogongana kwenye eneo moja la ulinzi, wakimuacha Mligo peke yake katika hali ya 2v1 dhidi ya winga na beki wa Gor Mahia. Pia, Simba wanahitaji kujua nani anashuka kuchukua mpira, nani anafanya movement mbele, ili wasimuache mshambuliaji wa kati akiwa peke yake dhidi ya mabeki wa timu pinzani.
Hata hivyo, jambo la kutia moyo ni kwamba Simba wana kikosi kipana. Hii inampa Fadlu nafasi ya kutuma ujumbe kwa kila mchezaji: “Yule atakayeonesha utayari na kuelewa majukumu yake mapema ndiye atakayecheza.” Katika soka, matokeo ni jambo la msingi – hakuna nafasi ya kusubiri sana.
Kwa ujumla, bado si rahisi kupata picha halisi ya ubora wa kikosi kwa sasa. Lakini muda haupo wa kutosha, hivyo kasi ya maandalizi lazima iongezeke. Mashabiki wa Simba wameonesha upendo mkubwa kwa timu yao, hasa kwenye Simba Day – ni jambo la kujivunia. Sasa ni zamu ya timu kujibu mapenzi hayo kwa kujituma zaidi kuelekea mashindano.