CREMONA: MSHAMBULIAJI wa zamani wa Leicester Jamie Vardy amesema “umri ni namba tu” wakati huu anapofungua ukurasa mpya wa maisha yake ya soka akiwa na klabu ya Cremonese inayoshiriki ligi kuu ya Italia Serie A.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 38, ambaye anatajwa miongoni mwa wachezaji wakubwa zaidi wa Leicester, aliondoka katika klabu hiyo mwishoni mwa msimu uliopita, akimaliza safari ya miaka 13 katika klabu ambayo aliifungia mabao 200 katika mechi 500, mabao 24 katika msimu wao wa ubingwa wa EPL 2015/16
Vardy amesajiliwa na timu hiyo mpya iliyopanda daraja hadi Serie A kwa uhamisho huru mapema mwezi huu na anaweza kucheza mechi yake ya kwanza klabuni hapo Jumatatu, klabu hiyo itakapokuwa uwanjani dhidi ya Verona.
Alipoulizwa na wanahabari kama yeye, na wakongwe wengine kama Kevin de Bruyne na Luka Modric ambao pia wamehamia Serie A msimu, bado wana ari ya kucheza kwa kiwango cha juu, alijibu:
“Lazima wewe ni mmoja wa watu wenye mashaka. Basi utakuwa mmoja wa watu nitakaowashangaza. Kwangu umri ni namba tu. Ilimradi miguu yangu inafanya kazi kama ilivyokuwa ikifanya awali na bado niko kama ‘fresh’ wao (Kevin de Bruyne na Luka Modric) basi nitaendelea”.
“Kwa sasa hakuna dalili za wao kupunguza kasi kwa hiyo nitaendelea na nitafanya kila kitu kwa ajili ya klabu hii. Nitajifunza Kiitaliano, lakini [kwa sasa] sio tatizo soka lina lugha yake,” alisema Vardy.
Cremonese wamekuwa na mwanzo mzuri wa msimu huu wa Serie A, wakifungua kampeni yao kwa ushindi uliowaacha wengi midomo wazi wa mabao 2-1 dhidi ya AC Milan kabla ya kuwalaza Sassuolo 3-2.
The post “Umri ni namba tu” – Vardy first appeared on SpotiLEO.