MANCHESTER: MLINDA mlango wa Manchester City Gianluigi Donnarumma amesema hana wasiwasi juu ya ushindani wa namba klabuni hapo baina yake na James Trafford akisema ushindani wenye afya utaibua ubora zaidi kwa wote wawili.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Italia alisajiliwa kutoka Paris St Germain kwa mkataba wa miaka mitano katika siku ya mwisho ya dirisha la usajili, na kusababisha maswali kuhusu nani atakuwa golikipa namba moja baada ya kuondoka kwa Ederson.
Trafford, aliyesajiliwa mapema kwenye dirisha hili, alianza katika mechi zote tatu za Ligi Kuu msimu huu lakini amekuwa chini ya shinikizo la mashabiki baada ya kufanya makosa mengi katika mechi waliopoteza mabao 2-0 dhidi ya Tottenham Hotspur.
“Nina furaha kwa sababu ushindani ni mzuri kwa kila mtu. Sina wasiwasi hata kidogo bali nina shauku ya kukutana naye (Trafford), na kukutana na wachezaji wenzangu wapya,” Donnarumma alikiambia chombo cha habari cha klabu.
“Lazima tuwe timu imara na yenye umoja, huo ndio ufunguo wa mafanikio. Kwa pamoja tunaweza kupata mafanikio makubwa. Siku zote nimekuwa na ndoto ya kucheza Ligi ya England, ni ligi bora zaidi duniani” – mchezaji huyo aliongeza.
Donnarumma anaweza kuwa kwenye nafasi ya kucheza mechi yake ya kwanza, Man City watakapoikaribisha Manchester United kwenye EPL Jumapili. City ipo nafasi ya 13 na pointi tatu katika mechi tatu walizocheza.
The post Donnarumma hana wasiwasi Man city first appeared on SpotiLEO.