Kiungo mshambuliaji wa Azam FC na timu ya Taifa ya Tanzania, Feisal Salum maarufu kama FeiToto, ameongeza kandarasi yake ya kuitumikia klabu hiyo kwa msimu mmoja zaidi. Hatua hiyo inamaanisha kuwa FeiToto atasalia ndani ya viunga vya Chamazi hadi mwaka 2027.
FeiToto, ambaye ni mmoja wa viungo bora nchini, ameendelea kuwa nguzo muhimu katika kikosi cha Azam FC kutokana na uwezo wake mkubwa wa kutawala eneo la kiungo na kutoa msaada katika safu ya mashambulizi. Uamuzi wa Azam kumwekea mezani kandarasi mpya unatajwa kuwa ni mkakati wa kuhakikisha nyota huyo anaendelea kuisaidia timu katika harakati zake za kutafuta mataji ya ndani na mafanikio ya kimataifa.
Kwa mujibu wa taarifa, kulikuwa na timu kadhaa zilizoonesha nia ya kumsajili FeiToto, lakini Azam FC imeamua kumuweka klabuni kwa muda mrefu zaidi, jambo linaloashiria imani kubwa waliyonayo kwa mchango wake. Hatua hii pia ni faida kwa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, kwani mchezaji huyu ataendelea kupata mwendelezo mzuri wa kucheza katika kiwango cha juu.