MADRID: MENEJA wa Atletico Madrid Diego Simeone yuko chini ya shinikizo kubwa kufuatia mwanzo mbaya wa klabu hiyo Atletico Madrid msimu huu huku kocha huyo akisaka ushindi wake wa kwanza msimu.
Colchoneros wako katika nafasi ya 17 kwenye LaLiga wakiwa na pointi mbili pekee katika michezo mitatu, nafasi mbaya kwa klabu iliyotumia takriban euro milioni 200 katika usajili wa majira ya kiangazi wakiwemo Alex Baena, Thiago Almada, David Hancko na Johnny Cardoso.
“Kushinda kungekuwa ahueni, huo ndio ukweli. Ningejisikia faraja nina jukumu kubwa kuhakikisha hilo,” Simeone aliuambia mkutano na wanahabari siku wakati kikosi chake kikijiandaa kuwakaribisha Villarreal walio juu kwenye msimamo.
“Katika kipindi cha miaka 14 iliyopita, tumejenga jina letu kwa ukubwa sana, na lazima tuudumishe ukubwa huo. Niko katika nafasi ambayo mimi ndiye mtu anayefuatiliwa kwa karibu zaidi, na sina budi kukubali hilo.” amesema Simeone
Shinikizo linazidi kupanda kwa Simeone, ambaye anaingia msimu wake wa 14 kwenye usukani wa klabu hiyo huku kukiwa na ukame wa miaka minne wa ubingwa na matarajio makubwa kufuatia uwekezaji mkubwa wa klabu hiyo majira ya kiangazi. Atletico wanajikuta wakiwa nafasi moja tu juu ya eneo la kushushwa daraja, mbali na matarajio makubwa waliyokuwa nayo.
Wapinzani wao wa Jumamosi, Villarreal wanawasili Madrid wakiwa wamekaa katika nafasi ya tatu wakiwa na pointi saba, mbili tu nyuma ya vinara Real Madrid na Athletic Bilbao walio nafasi ya pili.
Kocha huyo raia wa Argentina alikiri kwamba timu yake lazima irejeshe imani ya wafuasi lakini akawataka waaminifu kuunga mkono timu hiyo inayokabiliwa na matatizo. “Msaada wao utakuwa muhimu sana Jumamosi,” Simeone alisema.
The post Simeone ahaha kuinasua Atl. Madrid first appeared on SpotiLEO.