ARUSHA – Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imeiwezesha kampuni ya maziwa Galaxy Food and Beverages Ltd kuondoa vikwazo vya uzalishaji na kupanua masoko ya bidhaa zake za Kilimanjaro Fresh, hatua inayoongeza ajira na kuimarisha mnyororo wa thamani wa maziwa nchini.
Meneja wa uzalishaji wa Galaxy, Augustine Lyana, alisema kuwa kabla ya ushirikiano na TADB, kiwanda kilikabiliwa na changamoto za uwezo mdogo wa kusindika maziwa, utegemezi wa wafugaji wa nje kwa maziwa ghafi na upungufu wa usambazaji nje ya mkoa wa Arusha. “Changamoto hizi zilikuwa zinazuia kasi ya ukuaji wa kampuni,” alisema.
Kupitia uwezeshaji wa TADB, Galaxy imeanzisha shamba la kisasa lenye ng’ombe 240 wa maziwa, imeongeza laini ya uzalishaji kwa mashine ya UHT ya kisasa, na kupanua usambazaji wa bidhaa kutoka Arusha hadi Dar es Salaam, Dodoma na Mwanza, huku ikilenga kuingia katika soko la Afrika Mashariki.
“Ushirikiano huu umeleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kijamii,” aliongeza Lyana. “Tumeongeza ajira kwa vijana zaidi ya 200 wengi wao wanawake, kuboresha ubora na usalama wa maziwa, na kuimarisha mnyororo wa thamani wa sekta ya maziwa. Sasa Tanzania ipo tayari kushindana kwenye soko la kikanda kwa viwango vya kimataifa.”
Sekta ya maziwa nchini bado ina fursa kubwa. Takwimu za Wizara ya Mifugo zinaonyesha Tanzania huzalisha takribani lita bilioni 3 za maziwa kwa mwaka, lakini ni asilimia 12 pekee ndiyo husindikwa viwandani. Wataalamu wanasema kiwango kidogo cha usindikaji kimekuwa kikikwaza uwezo wa nchi kutumia kikamilifu rasilimali za mifugo na kuongeza thamani ya mazao ya maziwa.
Kwa sasa Galaxy inasindika maziwa safi, mtindi, yogurt, samli na jibini, na inalenga kutumia nguvu mpya ya uzalishaji kuingia kwenye masoko mapana ya Afrika Mashariki. Wataalamu wa sekta wanasema mafanikio ya kampuni hiyo yanaonyesha jinsi uwekezaji wa kimkakati unavyoweza kubadilisha kilimo-biashara na kuchochea ukuaji wa viwanda vya ndani.