Mgombe Ubunge wa Jimbo la Peramiho Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma Jenista Mhagama kulia,akimtambulisha kwa wananchi Mgombe Ubunge wa Jimbo la Madaba Mkoani humo Omari Msigwa maarufu Super Feo kwenye Mkutano wa kamapeni ya Ubunge Jimbo la Madaba uliofanyika katika kijiji cha Mtyangimbole Wilayni Songea.
Mgombea Ubunge Jimbo la Peramiho Mkoani Ruvuma Jenista Mhagama aliyelala chini na Mgombea Ubunge Jimbo la Madaba Omari Msigwa(Super Feo)wakimuombea kura Mgombea Urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi Rais Samia Suluhu Hassan kwenye Mkutano wa Kampeni ya Chama hicho uliofanyika katika Kijiji cha Mtyangimbole Wilayani Songea.
Katibu wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Ruvuma Mohamed Halfan kulia,aimkabaidhi Ilani ya Uchaguzi ya Chama hicho Mgombea Ubunge Jimbo la Madaba Omari Msigwa maarufu Super Feo wakati wa Mkutano mkubwa wa kampeni ya Udiwani,Ubunge na Urais uliofanyika katika Kijiji cha Mtyangimbole Wilayani Songea .
…………
Na Mwandishi Wetu, Ruvuma
KATIBU wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Ruvuma Mohamed Halfan, amewataka wananchi wa Jimbo la Madaba Wilayani Songea,kutofanya makosa kwa kuwachagua viongozi wa upinzani,badala yake wahakikishe wanachagua wagombea wa Chama hicho ambao wana dhamira ya kweli katika kuwaletea maendeleo.
Halfan, ametoa kauli hiyo jana wakati akimnadi Mgombe Ubunge wa Jimbo la Madaba kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi Omari Msigwa maarufu Super Feo kwenye uzinduzi wa Kampeni ya Ubunge iliyofanyika katika Kijiji cha Mtyangimbole kata ya Mtyangimbole.
Alisema,Msigwa ni mtu sahihi kwa maendeleo ya Jimbo la Madaba na Mkoa wa Ruvuma, kwani kupitia kampuni yake ya Super Feo&Selou Express ameajiri zaidi ya vijana 500 hivyo kuisaidia Serikali kupunguza changamoto kubwa ya ajira kwa Watanzania.
Amewaomba wananchi wa Madamba na Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla, kuwachagua na kuwapigia kura nyingi wagombea wa Chama hicho hata kwenye maeneo ambayo wapinzani hawajajitokeza kuchukua fomu kuomba Udiwani,Ubunge na Urais.
Halfan alisema,Serikali ya Chama cha Mapinduzi katika kipindi cha miaka minne Mgombea wake wa Urais Samia Suluhu Hassan,amepeleka fedha nyingi katika Jimbo la Madaba kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo mradi mkubwa wa maji Mtyangimbole utaogharimu zaidi ya Sh.bilioni 5.5.
Alisema,mradi huo ambao utekelezaji wake uko hatua ya mwisho utakapokamilika utakwenda kumaliza kabisa changamoto kubwa ya maji katika vijiji vitatu vya kata ya Mtyangimbole na vijiji viwili vya kata ya jirani ya Gumbiro.
Kwa mujibu wa Halfan licha ya mradi huo,Pia Serikali kupitia Wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)inaendelea kutekeleza Programu maalum ya uchimbaji visima 900-5 kila Jimbo ambapo Jimbo la Madaba limepata visima vitano ambavyo vimewezesha kupunguza changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi.
Alisema,wananchi wana kila sababu ya kumchagua tena Rais Samia Suluhu Hassan kwa sababu katika kipindi cha miaka minne amewezesha vjiji vyote vya Mkoa wa Ruvuma kufikiwa na nishati ya umeme na sasa kazi inayoendelea ni kuhakikisha umeme unafika kwenye vitongoji.
Kuhusu Kilimo, Halfan amewahaidi wananchi wa Madaba hususani wakulima kuwa Chama cha Mapinduzi kitahakikisha kina isimamia Serikali kuleta pembejeo za kutosha hasa mbolea za ruzuku ili wakulima wapate kwa bei nafuu na kuwawezesha kulima kwa tija.
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Madaba Omari Msigwa(Super Feo)amewaomba wana Madaba kujitokeza kwa wingi kwenye mikutano ya kampeni ya wagombea wa Chama cha Mapinduzi ili wapate fursa ya kusikia sera na ahadi za Chama hicho kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba mwaka huu.
Super Feo alisema,iwapo atachaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Madaba ataisimamia Serikali ili iweze kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa vitendo hususani kwenye miradi mbalimbali ili kuharakisha maendeleo ya Wananchi wa Jimbo hilo.
Naye Mgombea Ubunge wa Jimbo la Peramiho Jenista Mhagama, amekipongeza Chama cha Mapinduzi kwa mara ya kwanza tangu Nchi ipate Uhuru kumsimamisha mwanamke Dkt Samia Suluhu Hassan kuwa Mgombea Urais wa Tanzania.
“Chama cha Mapinduzi kimemteua mtu sahihi sana kwani Mama Samia ni mtu mahiri,makini na mwenye sifa kubwa ya kuwa Kiongozi wa Nchi yetu,nawaomba Watanzania wenzangu tumuunge mkono kwa kumpa kura nyingi tarehe 29 mwezi ujao”alisema Mhagama.
Aidha, amemshukuru Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Taifa na Mgombe Urais wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan, kwa kumteua Balozi Emanuel Nchimbi kuwa Mgombea Mwenza kutoka Mkoa wa Ruvuma.
“Rais Samia na Mwenyekiti wetu wa Chama cha Mapinduzi Taifa,ametupa heshima kubwa sisi Wananchi wa Mkoa wa Ruvuma kwa kumteua ndugu yetu mwana Ruvuma mwenzetu kuwa Mgombea mwenza,nawaomba sana wana Ruvuma tumpe kura nyingi siku ya terehe 29 Oktoba mwaka huu”alisisitiza Mhagama.
Alisema,katika kipindi kifupi cha miaka minne Rais Samia Suluhu Hassan ameendelea kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa vitendo kwa kupunguza kama siyo kumaliza kabisa changamoto ya upatikanaji wa huduma mbalimbali za kijamii zikiwemo huduma ya majisafi na salama chini ya Kauli Mbiu ya kumtua Mama ndoo kichwani.
Kwa mujibu wa Mhagama,wakati Rais Samia anaingia madarakani mwaka 2021 wakulima walikuwa wananunua mbolea kati ya Sh.100,000 hadi 150,000 lakini sasa bei ya mbolea imeshuka hadi kufikia Sh.65,000 hadi 70,000 mfuko mmoja.
Mhagama alieleza kuwa,kabla ya Rais Samia Suluhu Hassan hajaingia madarakani Mkoa wa Ruvuma ulikuwa unapokea tani 33,000 tu za mbolea lakini kwa sasa Mkoa huo unapokea zaidi ya tani 120,000 ambazo zimesaidia kukua kwa uchumi wa Mkoa wa Ruvuma na kuharakisha maendeleo ya wananchi.
Amewataka Wananchi Mkoani Ruvuma na Watanzania wote,kuhakikisha wanadumisha amani,utulivu na mshikamano wakati huu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Madiwani,Wabunge na Rais.
Mkazi wa Kijiji cha Mtyangimbole John Komba,ameishukuru Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi kwa uamuzi wa kumteua Omari Msigwa kuwa Mgombea Ubunge wa Jimbo la Madaba huku akieleza kuwa ni mtu sahihi na mchapakazi,mnyenyekevu na mwenye kuelewa shida za wananchi.
“Tunaishukuru sana Kamati Kuu,imetusikiliza sisi wana Madaba,tumempata mtu sahihi mwana wa nyumbani tunaamini atatufikisha mbali zaidi alisema Komba.