Uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) umefanya kikao muhimu na viongozi wa kimila (Laigwanan) pamoja na serikali za vijiji vya Enduleni, Kakesio na Nasporiong kujadili changamoto za kijamii na za uhifadhi zinazozikabili jamii za eneo hilo.
Katika mazungumzo hayo, moja ya hoja kuu iliyoibuliwa ni upungufu mkubwa wa maji kwa mifugo na wanyamapori hasa katika kipindi cha ukame kikali kinachotokea kati ya mwezi Agosti na Novemba. Viongozi hao walitambua umuhimu na uzito wa changamoto hiyo na wakakubaliana kuendelea kufanya vikao vya pamoja kwa lengo la kutafuta suluhu za kudumu.
Ushirikiano huu unatajwa kuwa hatua muhimu katika kuimarisha uhusiano kati ya jamii za wenyeji na mamlaka ya uhifadhi, huku ukihakikisha kwamba mahitaji ya binadamu na uhifadhi wa wanyamapori vinaendelea kupewa kipaumbele katika mustakabali wa Ngorongoro.