Mgombea Ubunge Jimbo la Songea Mjini na Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro, amesema utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020–2025 umekamilika kwa mafanikio makubwa, hususan katika sekta za kilimo, elimu, afya, maji na miundombinu.
Akizungumza kwenye mkutano wa uzinduzi wa kampeni katika jimbo la Songea Mjini uliofanyika uwanja ya shule ya msingi Kiburang’oma Kata ya Lizaboni, Dkt. Ndumbaro amebainisha kuwa mafanikio hayo ni pamoja na upatikanaji wa mbolea ya ruzuku, soko la mahindi kupitia NFRA, uboreshaji wa huduma za kijamii, pamoja na ukarabati wa uwanja wa ndege wa Songea.
Kuhusu Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2025–2030, Dkt. Ndumbaro amesema CCM imejipanga kusambaza umeme katika kila nyumba, kuendeleza ruzuku ya mbolea, kuhakikisha ardhi yote inapimwa na wananchi wanajenga kwenye viwanja vilivyopimwa, pia ameahidi ujenzi wa vyuo vikuu, masoko mapya ikiwemo Manzese A na B, pamoja na maghala ya kuhifadhia nafaka.
Katika sekta ya miundombinu, amesema barabara za mjini Songea zitaendelezwa kwa kiwango cha lami, zikiwemo Mtwara Korido, barabara ya Londoni–Subira, Msamala–Mwengemshindo, n.k, huku uwanja wa ndege ukiwekewa taa za kisasa kuruhusu ndege kutua usiku.
Aidha, Dkt. Ndumbaro amesema serikali itaboresha michezo kwa kuwekeza zaidi katika timu ya Manispaa ya Songea, Songea United, ili kuongeza hamasa na kuinua vipaji.
Amesisitiza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo utaiwezesha Songea kupanda hadhi na kuwa Jiji ndani ya kipindi cha miaka mitano ijayo, akibainisha kuwa Songea kwa sasa ni miongoni mwa miji inayokua kwa kasi zaidi Tanzania na Barani Afrika.
“Wananchi wenzangu wa Jimbo la Songea Mjini, kwa heshima na unyenyekevu mkubwa nawaomba mnipigie kura katika Uchaguzi Mkuu ujao ili tuendelee kushirikiana katika safari ya maendeleo.
Tumeweka msingi imara kupitia utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2020–2025, na sasa tunahitaji kuendeleza jitihada hizi katika Ilani mpya ya 2025–2030″.
Elibariki Emmanuel Kingu, kutoka Ikungi Mkoani Singida, amempongeza Mgombea Ubunge Jimbo la Songea Mjini Dkt. Damas Ndumbaro kwa uongozi wake thabiti ndani ya serikali ya awamu ya tano na sita, akisema ameonyesha mfano bora wa kizalendo na uadilifu katika kutumikia nafasi mbalimbali alizopangiwa.
Amesema mageuzi makubwa yaliyofanyika kwenye sekta ambazo Dkt. Ndumbaro amepitia ni ishara ya uthubutu na uzalendo wa kweli, hali inayomfanya kuamini kuwa wananchi wa Songea wanapaswa kuendelea kumuamini na kumpa nafasi ya kuendelea kuwatumikia.
Aidha, Elibariki amewataka wananchi wa Songea kutofanya kosa la kumchagua mgombea mwingine, akibainisha kuwa kura kwa Ndumbaro ni kura ya maendeleo, mshikamano na mustakabali bora wa taifa.
Awali akifungua mkutano wa kampeni Katika Jimbo la Songea Mjini, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Songea Mjini Mwinyi Msolomi, amesisitiza kuwa CCM ndicho chama pekee chenye mtandao wa uongozi kuanzia ngazi ya shina hadi taifa, amefafanua kuwa kumchagua mgombea wa chama kingine ni sawa na kumpa mtu nyumba bila ramani.
Aidha, amewataka wananchi wa Songea kumchagua Dkt. Ndumbaro, wakizingatia rekodi yake ya utendaji bora kuliko kuchagua mtu mpya kutoka chama kingine ambaye hawana uhakika na utendaji wake wa kazi.
Kwa upande wa waliokuwa watia nia wa ubunge kupitia CCM katika mchakato wa ndani ya chama, Legan Mbawala na Shakira Mohamed Shad wameungana na Watia nia wengine, kumuunga mkono Dkt. Ndumbaro wakisisitiza kuwa kazi zake katika awamu iliyopita zinaonyesha uwezo wake.
Wamewaomba wananchi wajitokeze kwa wingi tarehe 29 Oktoba kupiga kura kwa Rais, Mbunge na Madiwani wote wa CCM, kwa imani kuwa chama hicho kitaendeleza maendeleo na kuwatetea wananchi wa ngazi zote.