KIGALI:WACHEZAJI chipukizi wa Tanzania, Ngowamo Glory na Katamboya Rose, wameibuka mashujaa baada ya kung’ara katika Mashindano ya vijana chini ya umri wa miaka 16 ya Afrika yaliyofanyika Kigali, nchini Rwanda.
Ngowamo alitwaa tuzo ya ‘Best 3-Point Shooter’ kwa kufunga mitupo ya mbali 17, huku Katamboya akiteuliwa kuingia kwenye ‘Best Five Selection’ ya mashindano, ishara ya kiwango cha juu cha mchezo aliokionyesha.
Timu ya Taifa ya Kikapu ya Wasichana U16 (Taifa Stars wa Kikapu) ilimaliza mashindano hayo katika nafasi ya tano kati ya timu 11, mafanikio yanayochukuliwa kama hatua kubwa ya maendeleo ya mchezo huo nchini.
Kwa mara ya kwanza Tanzania imeweza kutoa wachezaji waliotambulika katika tuzo binafsi za FIBA barani Afrika, jambo linaloashiria kuibuka kwa kizazi kipya cha mabinti wenye vipaji vikubwa vya kikapu.
Mashabiki na wadau wa mchezo huo wamewapongeza wachezaji hao kwa kufanya vizuri wakisema matokeo hayo yameweka msingi wa matumaini mapya kwa mchezo wa kikapu nchini, huku wakiisifu serikali na Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF) kwa juhudi za kukuza mchezo huo.
The post Ngowomo, Katamboya wang’ara Kikapu Afrika first appeared on SpotiLEO.