DAR ES SALAAM; MREMBO maarufu wa muziki wa Bongo Fleva, Zuhura Othman ‘Zuchu’, amezungumzia kwa uwazi uhusiano wake wa karibu na Diamond Platnumz, ambaye ni mume wake na pia bosi wake katika lebo ya WCB Wasafi.
Katika mahojiano maalum na BBC, Zuchu amekanusha uvumi kuwa anapanga kuondoka WCB, akisisitiza kuwa hana sababu ya kufanya hivyo.
“Sidhani kama naweza kuondoka, maana boss ninaye chumbani kwangu,” amesema Zuchu kwa ucheshi, akithibitisha kuimarika kwa mahusiano yao ya kimapenzi na kikazi.
Zuchu alieleza kuwa licha ya kuwa sehemu ya lebo kubwa inayosimamiwa na mume wake, anajitegemea kwa kiasi kikubwa katika kazi zake.
Alifafanua kuwa WCB humsaidia kwa kumpatia rasilimali, lakini kazi ya kuleta matokeo ni yake binafsi.
“Ukiwa unafanya kitu unachokipenda, huoni kama ni utumwa,” ameongeza.
Kuhusu maisha ya ndoa na jinsi yanavyoathiri kazi yake, Zuchu alikiri kuwa vipaumbele vyake vimebadilika kidogo baada ya ndoa.
Amesema kuwa sasa anamheshimu zaidi mume wake akiwa nyumbani, japokuwa wakati mwingine wanalazimika kutenganisha masuala ya kazi na maisha binafsi.
“Mzee akiwa nyumbani, yeye ndiye namba moja. Wakati mwingine nakuwa na malalamiko yangu ya lebo, lakini ananiambia: ‘Hapana, mimi ni mume, siyo bosi’,” amesema kwa tabasamu.
Kauli hizi zinaonesha jinsi Zuchu anavyofanikiwa kusawazisha maisha ya ndoa na kazi, huku akidumisha nidhamu, upendo, na uwajibikaji katika pande zote mbili za maisha yake.
The post Zuchu afunguka kuhusu maisha yake ya ndo first appeared on SpotiLEO.