DAR ES SALAAM: Msanii nyota wa muziki wa Bongo Fleva, Zuhura Othuman ‘Zuchu’, amesema kuwa tayari amejitayarisha kiakili kuwa mama, lakini akisisitiza kuwa majukumu ya malezi ya mtoto wake hayatomuelemea, kwani ana familia kubwa itakayomsaidia hususan bibi yake.
Akizungumza kwa ucheshi na kujiamini, Zuchu alisema:
“Ndio (Yes), nimejitayarisha kiakili kuwa mama, lakini nina familia kubwa.
Sidhani kama huyo mtoto atapata tabu, nitamtupa huko kwa bibi yake mimi niwe huko jukwaani.”
Zuchu aliongeza kuwa mama yake mzazi amekuwa na mtazamo tofauti kuhusu mpango huo:
“Mama anasema, ‘Wee, nilivyokuzaa sikukupeleka kokote, lakini huyu mjukuu wake atapambana nae tu’,” alisema kwa kutabasamu.
Kauli ya Zuchu imeibua mjadala mpana kuhusu mfumo wa malezi ya watoto katika kizazi cha sasa, hasa kwa wanawake wanaojihusisha na kazi zinazohitaji muda mwingi kama muziki, uigizaji au biashara.
Kwa sasa, imekuwa kawaida katika familia nyingi za Kiafrika kuona mabibi wakibeba jukumu la kulea wajukuu wao, hali inayotofautiana na miaka ya nyuma ambapo mama mzazi ndiye aliyekuwa mlezi wa moja kwa moja wa mtoto wake.
Je, Ni Sawa Mtoto Kulelewa na Bibi Wakati Mama Yupo?
Spoti leo imezungumza na Mchambuzi wa masuala ya familia na malezi Catherine Karinga anasema kwamba, ingawa msaada kutoka kwa familia una umuhimu mkubwa, bado ni muhimu kwa mzazi hasa mama kuchukua nafasi ya moja kwa moja katika kulea mtoto wake.
Mtoto anapokua chini ya uangalizi wa bibi au ndugu wengine, anaweza kukosa ukaribu wa kihisia na mama yake mzazi, jambo ambalo linaweza kuwa na athari katika maendeleo yake ya kihisia na kijamii.
Kwa upande mwingine, kuna pendekezo kwamba wasanii na wanawake wengine wenye majukumu makubwa wanapaswa kujipa likizo ya uzazi (maternity break), si tu kwa afya zao, bali pia kuwapa watoto wao nafasi ya kupata malezi ya karibu kutoka kwao.
Zuchu ametoa kauli ya ujasiri inayowakilisha hali halisi ya wanawake wengi sio wote wa kisasa wanaojitahidi kusawazisha majukumu ya kazi na maisha ya kifamilia.
Hata hivyo, mjadala kuhusu nani anatakiwa kuwa mlezi mkuu wa mtoto bado unaendelea, na unahitaji tafakari ya kina kuhusu nafasi ya mama katika maisha ya mtoto
The post Zuchu: Nimejitayarisha kuwa mama first appeared on SpotiLEO.