LISBON: KITUO cha Televisheni cha Ureno RTP kimeripoti kuwa Klabu ya Benfica ya Ureno inatazamiwa kumtangaza Jose Mourinho kama meneja wao mpya kufuatia kutimuliwa kwa kocha wa kikosi hicho Bruno Lage baada ya kipigo cha mabao 3-2 mbele ya Qarabag kwenye mchezo wao wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Ulaya usiku wa kuamkia leo.
Benfica ilitoa taarifa ya kuachana na kocha Lage mara baada ya mchezo dhidi ya Quarabag ya Azerbaijan kumalizika kwa kipigo hicho cha aibu kutoka kwa timu ndogo inayoshiriki Ligi hiyo kwa mara ya pili katika historia.
Rais wa Benfica Rui Costa amenukuliwa akisema klabu hiyo itataja haraka mrithi wa Lage kabla ya mchezo wao wa ligi kuu ya Ureno dhidi ya AVS Futebol SAD Jumamosi huku kituo hicho cha TV kikisema tayari Rais huyo amefanya mazungumzo na ‘the special one’.
“Ningependa kumshukuru Bruno kwa kila kitu alichojaribu kufanya, kila kitu alichotaka kufanya na kila alichofanya Benfica, na kujitolea kwake mwaka mzima akiwakilisha klabu yetu,” Costa aliwaambia waandishi wa habari.
“Lakini, isivyo bahati, wakati umefika wa kuachana, na tunaamini ni wakati wa mabadiliko. Kuhusu kocha ajaye, ni wazi tunatumai kwamba Jumamosi Vila das Aves, tayari tutakuwa na kocha mpya kwenye benchi.”
Meneja wa zamani wa Chelsea, Real Madrid, Manchester United na Inter Milan Jose Mourinho hana timu baada ya kuondoka katika klabu ya Fenerbahce ya Uturuki mwishoni mwa mwezi Agosti, siku mbili baada ya timu yake kupoteza mechi ya playoff ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Benfica.
The post Benfica ‘wamvutia waya’ Mourinho first appeared on SpotiLEO.