* Watumika kwenye ujenzi wa miradi mikubwa kama Bandari ya Tanga, Bomba la Mafuta EACOP
* Tanga, Tanzania
Sekta ya Madini nchini inaendelea kushuhudia mageuzi ya kuongeza thamani madini yakiwemo ya ujenzi kama mchanga na kufungua fursa nyingine mpya kwa wachimbaji wadogo wa mchanga kupitia teknolojia bunifu za usindikaji.
Katika mkoa wa Tanga, Kampuni ya Muwa Trading Tanzania Limited imewekeza kwenye Kiwanda cha kuosha na kusafisha mchanga kwa maji ili kuondoa udongo na uchafu mwingine kama mizizi, hatua ambayo imebadilisha kabisa mtazamo wa thamani ya rasilimali hiyo kwa miaka mingi.
Kwa mkoa wa Tanga, unaojulikana kwa utajiri wa madini ya viwandani na ujenzi, mchanga safi unaopatikana baada ya kuoshwa sasa ni malighafi yenye thamani kubwa kwa viwanda vya saruji, miradi ya kimkakati ya Serikali ikiwemo Bandari ya Tanga na ujenzi wa Bomba la Mafuta la EACOP katika Kata ya Chongeleani.
Teknolojia hiyo pia inaelezwa kutoa fursa kwa wachimbaji wadogo na wawekezaji kuongeza mapato, kwa kuuza bidhaa iliyoongezewa thamani badala ya mchanga ghafi ambao unakuwa na bei ndogo ikilinganishwa na mchanga uliosafishwa.
Akizungumza na Madini Diary, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa Tanga Mhandisi Laurent Bujashi alieleza kuwa mchanga huo umeleta manufaa makubwa katika sekta ya viwanda na ujenzi mkoani humo.
“Mchanga unaosafishwa kiwandani hapa umetumika katika miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo ukarabati wa Bandari ya Tanga, ujenzi wa baadhi ya viwanda mkoani hapa, pamoja na utekelezaji wa bomba la mafuta ghafi kutoka Chongeleani, Tanga. Hatua hii si tu kwamba imerahisisha upatikanaji wa malighafi zenye ubora, bali pia imefungua soko jipya kwa wachimbaji na wafanyabiashara wa mchanga” alisitiza Bujashi.
Kwa upande wake, Afisa Uendeshaji wa kampuni hiyo, Kaparata Maulid, alieleza kuwa mchanga unaosafishwa una mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi ya mkoa na taifa kwa ujumla:
“Kupitia teknolojia hii tumefanikisha kutoa mchanga wenye ubora wa hali ya juu unaokidhi mahitaji ya miradi mikubwa ya kimkakati nchini. Hii ni hatua muhimu katika kuongeza thamani rasilimali zetu na kuunga mkono jitihada za Serikali za kujenga uchumi wa viwanda,” alisema Kaparata.
Alitaja baadhi ya faida za mchanga unaosafishwa kuwa ni pamoja na kuboresha ubora wa malighafi kwa miradi mikubwa ya miundombinu, kusaidia ujenzi wa viwanda vipya na ukarabati wa miradi, kutengeneza ajira kwa wakazi wa eneo husika sambamba na kutoa fursa ya soko endelevu kwa wachimbaji wadogo.
Kwa uwekezaji huo, Tanga inajipambanua kama kitovu cha uvumbuzi na thamani katika Sekta ya Madini, ikichangia moja kwa moja kwenye dira ya Tanzania ya kujenga uchumi shindani wa viwanda kupitia malighafi zinapatikana ndani ya nchi.