AMSTERDAM: KOCHA Christian Chivu wa Inter Milan amesema nahodha wa kikosi hicho Lautaro Martinez atafanyiwa vipimo vya mwisho vya utimamu wa mwili kabla ya kuamua kumchezesha kwenye mechi yao ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ugenini dhidi ya Ajax Amsterdam saa 4 usiku wa leo.
Mshambuliaji huyo wa Inter alitolewa akiwa na maumivu ya mgongo katika mchezo wa Dabi ya Italia walipopoteza kwa mabao 4-3 dhidi ya Juventus kabla ya mechi yao ya kwanza ya Champions League dhidi ya Ajax leo Jumatano.
“Tutamtathmini Lautaro tuone kama tutakuwa naye,” alisema Chivu, ambaye pia alipuuzilia mbali mapendekezo ya kutomtumia golikipa wa Uswizi Yann Sommer baada ya timu hiyo kuruhusu mabao sita katika mechi zao mbili zilizopita akiwa langoni.
“Sijafikiria kumbadilisha kipa. Si sawa kumweka Sommer na kumrushia mawe(kumtupia lawama). Sidhani kama ni vyema kwa mtazamo wa kibinadamu, Sommer alifanya kazi nzuri sana msimu uliopita ni mtu mwenye uzoefu, kwa thamani yake, anapaswa kusalia golini,” – Chivu alisema.
Akikizungumzia kikosi chake Chivu hakuonesha unyonge baada ya kufungwa na Juventus akisema mchezo huo uliwaimarisha zaidi licha ya kukosa matokeo akiwataka mashabiki wasitazame matokeo pekee bali maeneo mengine ambayo walifanya vizuri.
The post Lautaro kutathminiwa dhidi ya Ajax first appeared on SpotiLEO.