TANGA: MASHINDANO ya ngumi ya Klabu Bingwa Taifa yameanza mkoani Tanga ambapo jumla ya mabondia 97 kutoka mikoa mbalimbali wanatarajiwa kuchuana.
Kwa mujibu wa Rais wa Shirikisho la Ngumi Tanzania (BFT) Lukelo Willilo, mabondia hao wanatoka katika klabu 15 kutoka mikoa ya Tanga, Dar es salaam, Kagera, Arusha, Iringa na Dodoma.
Klabu zilizoshiriki ni MMJKT, Ngome, Magereza, Polisi Arusha, Tanga Central, Tanga Central B, Makorora, Kagera Boxing A na B, Iringa Boxing Club, General Chande, Band Coy, JKT Mgulani, Jeba na Amboni.
Mabingwa watetezi timu ya MMJKT (JKT Makao Makuu) wamejitapa kuendeleza ubabe wao katika mashindano kwa kujisifia mafanikio yao ya kutwaa Ubingwa huo mara nne mfululizo mbele ya mahasimu wao wa karibu timu ya Ngome.
Michuano hiyo itahitimishwa Septemba 20, 2025 ambapo wachezaji watakaofanya vizuri watawekwa kwenye hazina ya baadaye ya timu ya taifa kujiandaa na mashindano ya kimataifa.
“Mashindano haya tutaangalia viwango vya mabondia na vipaji vipya ambavyo vitatumika kwenye mashindano ya kimataifa hapo baadaye,”alisema Willilo.
The post Mabondia 97 kuchuana klabu bingwa taifa first appeared on SpotiLEO.