MADRID: BEKI wa Real Madrid Trent Alexander-Arnold anatarajiwa kuwa nje ya uwanja kwa wiki kadhaa kutokana na jeraha la misuli ya paja alilopata katika ushindi wa 2-1 wa Madrid dhidi ya Marseille kwenye Ligi ya Mabingwa jana Jumanne.
Alexander-Arnold alilazimika kufanyiwa mabadiliko dakika tano tu mchezoni katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu. Madrid imesema vipimo vilivyofanywa leo Jumatano vimeonesha kuwa mchezaji huyo wa kimataifa wa England ana “jeraha la kwenye misuli ya ‘biceps femoris’ katika mguu wake wa kushoto.”
Madrid imesema itatoa taarifa zaidi na bila kutoa ratiba rasmi ya kupona kwake.
Alexander-Arnold alikuwa akikimbia peke yake alipoinua na kuweka mkono nyuma ya mguu wake wa kushoto. Alianguka chini na kusubiri msaada wa matibabu na hatimaye nafasi yake ikachukuliwa na Dani Carvajal ambaye baadaye alitolewa kwa kadi nyekundu kwa kumpiga mpinzani kichwa na atakosa mechi inayofuata ya Ligi ya Mabingwa watakaposafiri hadi Kairat wiki mbili zijazo.
Alexander-Arnold alijiunga na Real Madrid kutoka Liverpool, akicheza kwa mara ya kwanza na klabu hiyo ya LaLiga kwenye Kombe la Dunia la Klabu. Aliisaidia Liverpool kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa na mataji mawili ya Ligi Kuu.
The post Trent kukaa nje wiki kadhaa first appeared on SpotiLEO.