
Mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka wananchi kudumisha amani na utulivu wakati wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.
Akizungumza Septemba 17, 2025 katika mkutano wa kampeni uliofanyika Kijiji cha Kajengwa, Makunduchi – Zanzibar, Dkt. Samia amesisitiza kuwa uchaguzi ni zoezi la kidemokrasia, hivyo wananchi wanapaswa kupiga kura kwa utulivu na kurejea nyumbani bila vurugu.
“Uchaguzi si vita, ni tendo la demokrasia. Niwaombe ndugu zangu, twende tukapige kura kwa utaratibu, turudi nyumbani ili nchi ibaki salama,” alisema Dkt. Samia huku akionya kwamba kushika silaha, iwe ya kijadi au ya kisasa, hakutaleta suluhu ya maana kwa taifa.
Dkt. Samia alihitimisha kwa kusisitiza kuwa amani ya Tanzania ni nguzo kuu inayopaswa kulindwa na kila Mtanzania hasa kipindi hiki cha uchaguzi.