PARIS: KOCHA wa Paris Saint-Germain (PSG) Luis Enrique, ameeleza sababu ya kutumia muda wote wa kipindi cha kwanza cha mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Atalanta akiwa kwenye chumba cha watangazaji (press room) kilichopo sehemu ya juu ya majukwaa ya mashabiki akisema kukaa huko kunampa ‘view’ nzuri zaidi ya kitu cha kurekebisha wakati wa mapumziko.
Ni mchezo wa pili mfululizo wa nyumbani Enrique ametazama kipindi cha kwanza akiwa juu kwenye majukwaa ya mashabiki badala ya eneo maalum la makocha (touchline) uwanjani hapo, baada ya kufanya hivyo dhidi ya Lens kwenye Ligue 1 Jumapili.
“Nimefanya kama nilivyofanya kwenye mechi iliyopita kwa sababu, kutokea juu, ninaona vitu vingi ambavyo ninaweza kuvirekebisha wakati wa mapumziko. Kujua mambo mengi zaidi ni muhimu sana kwangu.” – Luis Enrique alimueleza mtangazaji wa Canal Plus.
Luis Enrique alirejea kwenye ‘touchline’ kipindi cha pili
Katika mkutano wake na wanahabari wa kabla ya mechi, alieleza sababu ya mbinu yake hiyo mpya akisema inamsaidia kutazama mambo kwa njia ya kipekee zaidi. Makocha wa mchezo wa Rugby hutumia mbinu hii, ambapo husimama kwenye majukwaa badala ya uwanjani.
“Ni tofauti sana kutazama mchezo ukiwa chini. Mazungumzo yangu ya wakati wa mapumziko dhidi ya Lens yalikuwa tofauti kabisa kwa sababu nilikuwa pale juu. Niliona mambo ya kuboresha, makosa kadhaa,”
“Nimefikiria kwa muda mrefu jinsi tunaweza kuongeza kitu kwenye namna yetu ya kufanya mambo, na siku zote nimekuwa tayari kwa chochote ambacho kinaweza kuboresha utendaji wetu.” – alisema.
The post Enrique aanika sababu za kukaa kwa Mashabiki first appeared on SpotiLEO.