YANGA imeshatua Angola tayari kwa kukutana na Waliete FC, ya huko lakini kabla ya mastaa wa timu hiyo hawajashuka kwenye ‘pipa’ kuna mamilioni wameingiziwa ambayo yanatokana na Simba.
Yanga itakuwa uwanjani kesho, kupambana na Waliete ukiwa ni mchezo wa kwanza wa hatua ya awali ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na baada ya wiki moja timu hizo zitarudiana Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Hata hivyo, mabosi wa Yanga wamewapa mzuka wachezaji, kwa kuwapatia kiasi cha Sh200 milioni ambazo ni bonasi ya ushindi katika fainali ya Ngao ya Jamii dhidi ya Simba.
Inafahamika kuwa, Kabla ya mchezo huo mabosi wa Yanga waliwafuata wachezaji kambini ‘Avic Town’, kisha wakawaambia wanautaka ushindi dhidi ya Simba kisha ukapatikana wa bao 1-0.
Ushindi huo ulikuwa na ahadi, kama Simba ingefungwa basi wachezaji wangepewa kiasi cha Sh200 milioni, zitakazotolewa na bosi wa klabu hiyo Ghalib Said Mohammed ‘GSM’.
Taarifa za ndani zilisema kuwa “Mabosi wa Yanga hawakutaka kuchelewa, baada ya ushindi huo walimalizana fasta na wachezaji wao ili wapate mzuka wa kushinda ugenini kule Angola.
“Tuliwaahidi Sh200 milioni, kama wangeifunga Simba na tayari hizo fedha zipo kwenye akaunti zao tena hata kabla ya timu haijafika Angola.
Mmoja wa viongozi ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema; “Mambo ya kudaiwa bonasi tumeziachia timu ndogo, ndiyo maana mnaona tukiwaahidi wachezaji wanataka kufia uwanjani ili wapate chao, kwa kuwa wanajua hawacheleweshewi.”
SIMBA IMEPOTEZA 350
Wakati mabosi wa Yanga wakimaliza ahadi hiyo kibabe, kule Simba ni kilio kwani mastaa wamepoteza kuvuna jumla ya Sh350 milioni, kutokana na kipigo cha Yanga.
Staa mmoja wa Simba alisema kuwa “Kabla ya mchezo huo, uongozi wetu ulituahidi Sh250 milioni kama tungeshinda, lakini pia mzabuni wa jezi Jayrutty aliahidi Sh100 milioni kama wangeshinda.”
Ahadi hizo zote zimeyeyuka, kutokana na matokeo hayo ya kipigo cha bao 1-0, huku wakijipanga kuwang’oa Gaborone United ya Botswana.
Simba imeshatua Botswana na Jumamosi, Septemba 20 itakutana na Gaborone United kwenye mchezo wa mtoano wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya awali.
The post KISA SIMBA…..MASTAA YANGA WALAMBA MIL 200 ZA CHAP CHAP….DILI ZIMA LIKO HIZI…. appeared first on Soka La Bongo.