VIONGOZI wa Yanga wamefanya kila kitu kuhakikisha timu hiyo inaendelea kuwa na kikosi kizuri chenye uwezo wa kutetea mataji iliyobeba msimu uliopita ikiwamo Ligi Kuu Bara.
Yanga ikiwa ndiyo klabu yenye mafanikio zaidi katika Ligi Kuu Bara ikichukua taji hilo mara 31, inaingia msimu huu ikiwa na deni la kutetea ubingwa wake.
Katika kutetea ubingwa huo, majukumu yamewekwa chini ya benchi la ufundi linaloongozwa na kocha mkuu, Romain Folz, raia wa Ufaransa ambaye amekuja kuchukua nafasi ya Miloud Hamdi, aliyeondoka msimu uliopita ulipomalizika.
Hamdi hakuondoka Yanga kinyonge, licha ya kuingia katikati ya msimu, lakini alipambana kuhakikisha timu inaendeleza makali yake na kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara.
Rekodi zinaonyesha Yanga imebeba ubingwa wa ligi hiyo mara nne mfululizo ikiwa ni msimu wa 2021-22, 2022-23, 2023-24 na 2024-25. Kumbuka timu hiyo ilisitisha utawala wa Simba ambayo nayo ilikuwa imeshinda mara nne mfululizo ikisaka taji la tano.
Katika mataji hayo manne yaliyobebwa na Yanga mfululizo, makocha waliowezesha hilo ni Nasreddine Nabi (2021-22 na 2022-23), Miguel Gamondi (2023-24), Miloud Hamdi (2024-25).
Wakati akiwa na mzigo huo mkubwa unaomkabili mbele, kitendo cha Folz kuanza msimu na taji la Ngao ya Jamii kwa kuifunga Simba, inaonyesha mwanga mzuri kwake, lakini kilichobaki ni mwendelezo wa hayo mazuri.
Folz ambaye huu ni msimu wa kwanza kwake ndani ya Ligi Kuu Bara, alitambulishwa kuinoa Yanga Julai 14, 2025.
Kwa walichofanya watangulizi wake, moja kwa moja Folz ana kazi ya kufanya kuhakikisha timu hiyo inaendelea ubora uleule wa kubeba mataji. Hivyo ashindwe mwenyewe kufanikisha hilo.
DENI KUBWA
Katika msimu huu, Folz ana deni kubwa la kuhakikisha timu inatetea ubingwa, lakini pia kiwango cha kufunga mabao mengi kinaendelea kama ilivyokuwa msimu uliopita.
Yanga wakati inabebea ubingwa wa ligi msimu uliopita, ilifunga mabao 83 yakiwa ni mengi zaidi ya timu nyingine 15 ndani ya ligi hiyo. Hata msimu wa nyuma yake 2023-2024, timu hiyo iliongoza kwa mabao ikifunga 71. Lakini 2022-2023 licha ya kubeba ubingwa, haikuwa na mabao mengi kwani ilifunga 61, ikizidiwa na Simba iliyomaliza nafasi ya pili ikitikisa nyavu za wapinzani mara 75.
MAJEMBE MAPYA
Jambo la kwanza lililofanyika ndani ya Yanga, ni kuimarisha timu kwa kusajili wachezaji wapya baada ya kuondoka baadhi yao waliokuwa wakicheza kikosi cha kwanza.
Katika hilo, wamesajiliwa wachezaji 11 ambao ni Frank Assinki (beki wa kati), Mohamed Hussein (beki wa kushoto), Abubakar Nizar Othuman ‘Ninju’ (beki wa kati), Moussa Balla Conte (kiungo mkabaji), Abdulnassir Mohamed Abdallah ‘Casemiro’ (kiungo mkabaji), Mohamed Doumbia (kiungo wa mshambuliaji), Lassine Kouma (kiungo mshambuliaji), Offen Chikola (winga), Celestin Ecua (winga), Edmund John (winga) na Andy Boyeli (mshambuliaji).
Usajili wa majembe hayo ni katika kuziba mapengo ya wale walioondoka akiwamo Stephane Aziz KI ambaye ameuzwa kwenda Wydad Casablanca ya Morocco. Wengine ni Khalid Aucho, Clatous Chama, Kennedy Musonda na Jonas Mkude ambao mikataba yao imemalizika, huku Nickson Kibabage akipelekwa Singida Black Stars kwa mkopo.
WATU WA KAZI
Ndani ya kikosi cha Yanga kwa msimu wa 2025-26, kuna watu wa kazi 31 wakiwamo 12 wa kigeni ambao ni Djigui Diarra, Chadrack Boka, Frank Assinki, Moussa Balla Conte, Duke Abuya, Maxi Nzengeli, Lassine Kouma, Mohamed Doumbia, Andy Boyeli, Prince Dube, Pacome Zouzoua, Celestine Ecua.
Wazawa ni Khomeiny Abubakar, Aboutwalib Mshery, Israel Mwenda, Kibwana Shomari, Mohamed Hussein, Ibrahim Bacca, Bakari Mwamnyeto, Dickson Job, Abubakar Nizar ‘Ninju’, Aziz Andabwile, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Denis Nkane, Edmund John, Mudathir Yahya, Abdulnassir Abdallah ‘Casemiro’, Offen Chikola, Shekhan Khamis, Clement Mzize na Farid Mussa.
BENCHI LA UFUNDI
Hapa kuna sura nyingi mpya ambazo zimekuja na Folz akiwa Kocha Mkuu wa kikosi hicho. Wengine ni Manu Rodriguez (Kocha Msaidizi), Majdi Mnasria (Kocha wa Makipa), Tshephang Mokaila (Kocha wa Utimamu), Thula Bantu (Mchambuzi wa Video), Paul Matthews (Mkurugenzi wa Ufundi) na Youssef Ammar (Mtaalamu wa Viungo) aliyerejea baada ya kuondoka miezi michache iliyopita, huku Walter Harrison akiwa ni meneja wa timu ambaye ni mzawa akiwa na timu hiyo kwa msimu wa nne sasa.
The post KWA HILI…..FOLZ ASHINDWE MWENYEWE NA HII YANGA AISEE…. appeared first on Soka La Bongo.