Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Ismail Ali Ussi, ameweka jiwe la msingi katika wodi ya mama na mtoto katika Kituo cha Afya cha Mwami N’tale, kilichopo kata ya Heru, Halmashauri ya Mji Kasulu.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Ussi amesisitiza umuhimu wa wananchi kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu ujao kwa amani, utulivu, na kuchagua viongozi wanaowataka. Amesema kaulimbiu ya Mwenge wa Uhuru mwaka huu inahimiza amani kama msingi wa maendeleo ya taifa.
“Maendeleo tunayoyaona leo ni matokeo ya utulivu na amani inayotamalaki nchini. Hivyo ni wajibu wetu kuilinda na kuithamini hali hii,” alisema Ussi.
Mradi wa ujenzi wa kituo hicho umegharimu kiasi cha Tsh milioni 300, na tayari umekamilika kwa asilimia 100. Utaanza kutoa huduma za afya kwa kina mama na watoto katika eneo la Heru na maeneo jirani.
Kituo hiki kinatarajiwa kupunguza kwa kiwango kikubwa vifo vya mama na mtoto kwa kutoa huduma bora, za karibu, na za uhakika kwa wananchi.
Mwenge wa Uhuru umeendelea kuwa chombo muhimu katika kuhamasisha maendeleo, uwajibikaji, na uzalendo miongoni mwa Watanzania.