LIVERPOOL: MENEJA wa Atletico Madrid, Diego Simeone amelalamikia matusi kutoka kwa mashabiki wa Liverpool licha ya kukiri kuwa hatua ya kujibizana nao haikuwa busara baada ya kocha huyo kupewa kadi nyekundu kufuatia majibizano hayo baada bao la dakika za jioni la wenyeji wao kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa ulaya dimbani Anfield usiku wa kuamkia leo.
Muargentina huyo alishuhudia kikosi chake kikiweka sawa mzani wa matokeo ya mabao mawili kabla ya beki Virgil van Dijk kufunga kwa kichwa dakika ya 92 na kuwaacha Atletico na kichapo cha mabao 3-2 baada ya filimbi ya mwisho.
Simeone alionekana kukerwa na kujibizana na mmoja wa mashabiki wa Liverpool waliokuwa nyuma ya benchi lake la ufundi na hatimaye mwamuzi raia wa Italia Maurizio Mariani kumuonesha kadi nyekundu na kumuondoa uwanjani. Baadaye aliiambia Movistar kuwa alikuwa amevumilia matusi kwa dakika 90.
“Kumekuwa na matusi mechi yote, lakini mimi ndiye ninayepaswa kuwa mtulivu na kuvumilia kila kitu, matusi ya maneno, ishara, na kadhalika. (Liverpool) wamekuwa wakijitapa kufanya vizuri, lakini wanatukana muda wote wa mechi kukutoa kwenye reli na huwezi kusema chochote, kwa sababu mimi ndiye kocha” – alisema Simeone.
“Kujibishana nao kwa matusi hakukubaliki, lakini hujui hisia gani unapata kwa kutukanwa kwa dakika 90 bila kukoma. Na kwa kweli, goli la mpinzani linapokaribia unageuka na wanaendelea kukutukana, na kwa hali ile, kilichotokea ndicho kinachotokea.” – aliongeza
Alipoulizwa baadae wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari ni nini hasa kilizungumzwa kumkosesha utulivu, alisema hataki kugusia tena kilichotokea akisema ni kuupa nguvu mjadala wa ‘kipuuzi’.
The post “Nimetukanwa kwa dakika 90” – Simeone first appeared on SpotiLEO.