

Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na utawala bora (THBUB), Bw. Patience Ntwina amesema kuwa uchaguzi ni mchakato muhimu unaojegwa juu ya misingi ya demokrasia, uhuru na amani, hivyo ni wajibu wa kila taasisi kuhakikisha haki za binadamu zinalindwa, zinaheshimiwa na kutekelezwa kabla, wakati na baada ya uchaguzi.
Akizungumza leo Septemba 18, 2025 wakati wa ufunguzi wa mafunzo kuhusu uzingatiwaji wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora kwa Maafisa wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam, Bw. Ntwina alibainisha lengo la mafonzo haya kwa Jeshi la Polisi kwani ni wadau muhimu katika utekelezaji wa sharia na kuhakikisha usalama wa wananchi hususani katika kipindi hiki cha uchaguzi.
“Mafunzo haya yanalenga kuongeza uelewa wa Maafisa wa Jeshi la Polisi kuhusu nafasi yao katika kulinda haki za wananchi na kuhakikisha wananchi hao wanatimiza haki yao ya kikatiba ya kuchagua viongozi bila hofu” alisema Bw. Ntwina.

Aidha, alisisitiza kuwa katika kipindi hiki cha uchaguzi Jeshi la Polisi lina wajibu wa kujiepusha na migogoro isiyo ya lazima, badala yake kuhakikisha usalama wa watu na mali zao.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam, SACP Muliro Jumanne amesema mafunzo haya yataongeza kiwango cha uwajibikaji, taaluma, maadili pamoja na kuheshimu haki za binadamu.
“Kimsingi mafunzo haya yanatukumbusha kulinda na kuheshimu haki za binadamu na jinsi ambavyo utekelezaji sheria unaweza ukafanyika katika mazingira yaliyo salama, pia tumekumbushwa sote wananchi na wasimamizi wa sheria tuna wajibu kutimiza majukumu yetu kwa kuzingatia sharia za nchi” amaesema Kamanda Muliro.
