Na Neema Mtuka Sumbawanga
Rukwa:Vijana mkoani Rukwa wametakiwa kuchangamkia fursa zilizopo katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, uchimbaji wa madini na ujasiriamali, ili kujiinua kiuchumi na kuchangia katika maendeleo ya Taifa.
Wito huo umetolewa na Dafroza Msechu, aliyemuwakilisha Katibu Tawala wa Wilaya ya Sumbawanga, Gabriel Masinga, katika kongamano la vijana lililoandaliwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga.
Dafroza amesema vijana wanapaswa kuamka na kutumia rasilimali zilizopo mkoani humo, ikiwemo ardhi yenye rutuba na madini, ili kuongeza tija katika maisha yao binafsi na jamii kwa ujumla.
Kwa upande wake, Frank Mateni, Mkuu wa Kitengo cha Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Sumbawanga, aliyemuwakilisha Mkurugenzi wa Manispaa, amesema mafunzo yaliyotolewa kupitia kongamano hilo ni nyenzo muhimu kwa ustawi wa vijana na kujenga Taifa endelevu.
Naye Godruck Magova, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Manispaa ya Sumbawanga, amesema kongamano hilo ni hatua ya kwanza ya kuwafungulia vijana milango ya fursa mbalimbali ili waweze kutambua thamani ya rasilimali zilizopo ndani ya Halmashauri na mkoa mzima wa Rukwa.
Aidha, vijana walioshiriki kongamano hilo wameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga kwa kuandaa jukwaa hilo, wakisema litawasaidia kufikia ndoto zao na kujiwekea misingi imara ya kimaendeleo.