NA DENIS MLOWE, IRINGA
MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Iringa Mjini kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Fadhili Ngajilo amewahidi wananchi kuwa endapo watamchagua atakuwa mbunge anayewasilisha changamoto mbalimbali kwa serikali ziweze kutatuliwa.
Ngajilo amezungumza hayo wakati wa kampeni za kata kwa kata iliyofanyika katika eneo la Igeleke kata Mkimbizi aliambatana na mgombea udiwani wa kata hiyo Eliud Mvela kuwa atakuwa mbunge ambaye atashirikiana na wananchi katika kuleta maendeleo.
Alisema kuwa katika jimbo la Iringa mjini kuna changamoto tofauti hivyo endapo atakuwa mbunge atakuwa sautI ya wananchi katika vyombo vya maamuzi. Hususan bungeni.
Aidha aliongeza kuwa atakuwa daraja kati ya wananchi, serikali na vyombo vingine vya maendeleo na kuwa mhamasishaji wa maendeleo ya uchumi kama Miundombinu ya Barabara, masoko, usafi wa mji, utengenezaji Ajira na kuhamasisha Utalii.
Ngajilo alisema kuwa atakuwa kiungo wa utoaji huduma bora za Elimu, Afya, Michezo na Sanaa na kuwa nguzo ya usalama wa raia na mali zao, ulinzi dhidi ya ukatili wa watoto na ukatili wa kijinsia.
Vilevile alisema kuwa endapo watampa nafasi ya kuwa mbunge atakuwa mlezi wa kuyaunganisha makundi ya wajasiriamali kama Machinga, Maafisa uSafirishaji na vikundi vya maendeleo.
Aliwaahidi wakazi wa kata ya Mkimbizi Kuwa mbunifu katika kutumia fursa zinazoizunguka manispaa ya lringa mfano vivutio vya utalii, ujirani na Jiji la Dodoma, fursa za ardhi zilizopo Kilolo, Isimani na Kalenga, kuwepo wa vyuo vikuu vingi,
Alimalizia kueleza Kuwa Usukani kuelekeza manispaa kwenye utekelezaji wa kishindo wa ilani y uchaguzi 2025 – 2030, na Dira ya Taifa ya maendeleo 2025 – 2050.
Kwa upande wake mgombea udiwani kata ya Mkimbizi Eliud Mvela aliwaomba wananchi mkataba miaka 5 mengine ili aweze kukamilisha miradi ya maendeleo iliyoanzishwa ikiwemo ujenzi wa soko la kata Mkimbizi.
Alisema kuwa akichaguliwa kuwa diwani atahakikisha anatembea kwenye ilani ya chama na kutokwenda nje ya chama katika kuleta maendeleo ya kata.