NA DENIS MLOWE, IRINGA
WANANCHI wa kata ya Igumbilo iliyoko katika jimbo la Iringa mjini wamesema wako tayari kupiga kura katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu ili kumchagua Mgombea wa Urais kupitia CCM Dk Samia Suluhu Hassan na wabunge na madiwani.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa kampeni za mgombea ubunge jimbo la Iringa mjini Fadhili Ngajilo walisema kuwa habari za kupotosha watu kwamba hakuna uchaguzi ni za kupuuza hivyo wananchi watajitokeza kwa wingi katika kupiga kwani mambo aliyofanya mgombea wa CCM Mama Samia anastahili kurudi tena kuongoza nchi ya Tanzania.
Mmoja ya wananchi hao Mzee Mbosa ambaye ni mkazi wa Igumbilo alisema kuwa ifike wakati nchi inahitaji kiongozi bora hivyo sisi Iringa tutampa kura za kutosha.
Alisema kuwa kama ilivyokawaida mkoa wa Iringa tutakuwa wa kwanza kwa ushindi mkubwa kwa kura za rais
“Mwandishi Mkoa wa Iringa ni ngome ya CCM, na tutaiendeleza ngome hii kwa kumpa kura mama Samia na wabunge na madiwani katika Uchaguzi wa Oktoba mwaka huu ” Alisema
Naye Mgombea udiwani kata hiyo, Jackson Chatanda alisema kuwa mkoa wa Iringa wamekuwa mstari wa mbele kushiriki uchaguzi, kwani kuna kata ambazo waliojiandikisha hupiga kura wote isipokuwa wagonjwa na waliopoteza maisha hii ni ishara tosha kwamba mama Samia atashinda kwa kura nyingi.
Akizungumzia uongozi wa Dk. Samia, Chatanda alisema wananchi wa Iringa wanamkubali si kwa sababu ya jinsia yake, bali kwa uwezo na uongozi thabiti aliouonyesha.
Naye aliyekuwa meya wa Manispaa Iringa Mjiini Ibrahim Ngwada akimnadi Mgombea ubunge Fadhili Ngajilo alisema kuwa wamepata msahihi latika kushirikiana na baraza kuleta maendeleo.
Kwa Upande wake mgombea ubunge wa Jimbo la Iringa Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Fadhili Ngajilo, ameahidi kuboresha ofisi ya mbunge ili iwe na watendaji wasikivu watakaopokea na kushughulikia kero za wananchi kwa ufanisi, pindi atakapochaguliwa kuwa mwakilishi wa jimbo hilo
Alisema kuwa atakuwa mwepesi kukutana na wananchi kuweza kuwasikiliza na nitakuja kwenu mara nyingi na kutakuwa na ofisi ya mbunge itakayofikika na kila mwana-Iringa.
Alibainisha kuwa kipaumbele chake kitakuwa kushughulikia changamoto za vijana kwa kuhakikisha wanapata mikopo ya ujasiriamali yenye riba nafuu, na kutoa elimu ya ujasiriamali ili kuwezesha vijana kujiajiri kuliko kutegemea serikalini kupata ajira.





