LONDON: MENEJA wa Chelsea, Enzo Maresca amezua mjadala mitandaoni baada ya kutoa kauli zisizo za kawaida kuhusu sakata la wachezaji, Raheem Sterling na Axel Disasi waliotelekezwa na Kikosi hicho, akisema kuwa hali yao ni ya kawaida ikilinganishwa na ugumu wa maisha ya baba yake mzazi aliyekuwa mvuvi kwa miaka 50.
Winga Sterling na beki Disasi wanafanya mazoezi kando na kikosi cha kwanza cha Chelsea baada ya Maresca kuwatangaza wawili hao ambao walitoka kwa mkopo msimu uliopita sio sehemu ya mipango yake msimu huu.
Alipoulizwa iwapo afya yao ya akili inaweza kuathiriwa na mazoezi ya kujitenga na kula mbali na wachezaji wenzao, Maresca alisema: “Baba yangu ana umri wa miaka 75 na kwa miaka 50 amekuwa mvuvi, akifanya kazi kuanzia saa nane usiku hadi saa 4 asubuhi peke yake. Hii ndio ngumu maishani sio jinsi mchezaji anavyofanya kazi.”
Sterling na Disasi wana mikataba inayoendelea hadi 2026 na 2029, mtawalia, na Muitaliano huyo alikubali ugumu wa kulitatua suala lao huku akidumisha msimamo wake kifalsafa.
“Kama mchezaji, nimepitia hali kama ya Raheem na Axel na, kwa hakika, najua kwamba sio hisia nzuri kwa mchezaji. Unataka kufanya mazoezi na kucheza michezo,” Maresca aliwaambia waandishi wa habari.
Zaidi ya wachezaji 20 wameondoka Chelsea siku za karibuni lakini Sterling na Disasi walisalia klabuni hapo huku wawili hao wakiachwa nje ya kikosi cha Chelsea kinachocheza Champions league.
The post Maresca atoa kauli tata kwa Sterling na Disasi first appeared on SpotiLEO.