Mkuu wa Idara ya Masoko na Mauzo kutoka Oryx Gas, Bw. Shaban Fundi,Mkurugenzi na Mwanzilishi wa TCRF, Bi. Sarah Ngoma pamoja na wadau mbalimbali wakikata utepe ikiwa ni ishara ya uzindua wa jiko linalotumia mfumo wa nishati safi uliofanyika leo, Septemba 19, 2025, katika Shule ya Sekondari Yusuf Makamba, Dar es Salaam.
Mkuu wa Idara ya Masoko na Mauzo kutoka Oryx Gas, Bw. Shaban Fundi akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa jiko linalotumia mfumo wa nishati safi uliofanyika leo, Septemba 19, 2025, katika Shule ya Sekondari Yusuf Makamba, Dar es Salaam.
Mkurugenzi na Mwanzilishi wa TCRF, Bi. Sarah Ngoma akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa jiko linalotumia mfumo wa nishati safi uliofanyika leo, Septemba 19, 2025, katika Shule ya Sekondari Yusuf Makamba, Dar es Salaam.
……….
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Katika kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Kampuni ya Oryx Gas Tanzania kwa kushirikiana na Taasisi ya Tanzania Communities Rise Foundation (TCRF) wamezindua jiko linalotumia mfumo wa nishati safi, hatua inayolenga kupunguza matumizi ya mkaa nchini.
Uzinduzi wa jiko hilo umefanyika leo, Septemba 19, 2025, katika Shule ya Sekondari Yusuf Makamba iliyopo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkuu wa Idara ya Masoko na Mauzo kutoka Oryx Gas, Bw. Shaban Fundi, amesema kuwa jiko hilo litasaidia shule hiyo yenye jumla ya wanafunzi 1,391 kuachana na matumizi ya nishati isiyo rafiki kwa mazingira, hususan mkaa.
“Serikali imekuwa ikisisitiza matumizi ya nishati safi ya kupikia. Sisi kama Oryx Gas tumeona ni muhimu kuonesha mfano kwa vitendo kwa kufanikisha mradi huu wa kufunga mifumo ya nishati safi shuleni,” amesema Fundi.
Ameeleza kuwa majiko ya kisasa ya gesi siyo tu yanapunguza madhara ya kiafya yatokanayo na moshi, bali pia yanasaidia kuongeza ufanisi katika uandaaji wa chakula kwa taasisi zenye watu wengi kama shule. “Shule hii ina walimu, wapishi na wanafunzi wengi waliokuwa wakipata adha ya moshi. Kupitia TCRF, sasa wamepata suluhisho,” ameongeza.
Aidha, Fundi ametoa wito kwa wadau mbalimbali kufika Oryx Gas kwa ajili ya majadiliano kuhusu uwekaji wa mifumo ya nishati safi ambayo ni salama na inakidhi viwango vya ubora vya kitaifa na kimataifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi na Mwanzilishi wa TCRF, Bi. Sarah Ngoma, amesema taasisi hiyo imekuwa ikishirikiana na Oryx Gas katika miradi ya kueneza matumizi ya nishati safi, ikiwemo kuwawezesha mamalishe kutumia gesi badala ya mkaa.
“Tumekuwa tukitekeleza miradi hii katika mikoa mbalimbali ikiwemo Lindi, hususan vijijini. Tunaamini kupitia ushirikiano huu na kampuni kama Oryx, tutafanikisha malengo yetu kwa haraka,” amesema Ngoma.
Ameongeza kuwa TCRF ina kanzi data ya shule zaidi ya 10 zilizofanyiwa tafiti, zikiwemo shule zinazotegemea mkaa, kama Shule ya Sekondari Yusuf Makamba. “Tunaona athari za matumizi ya mkaa hazimuathiri mtumiaji wa moja kwa moja tu, bali hata jamii inayomzunguka,” ameeleza.
Ngoma amesema wameanza na shule ya Yusuf Makamba pamoja na Shule ya Sekondari Kiluvya, huku akitoa wito kwa wadau, mashirika na taasisi mbalimbali kusaidia jitihada hizi, hasa taasisi zenye mkusanyiko mkubwa wa watu.
“Kufungwa kwa jiko la Oryx katika shule hii ni neema kubwa. Tunatarajia litapunguza muda wa kupika na kuongeza ufanisi, hasa kwa kuwa wanafunzi ni wengi na mahitaji ya chakula ni makubwa,” amesema Ngoma.