Na Neema Mtuka Sumbawanga
Rukwa :Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Charles Makongoro Nyerere, ametoa wito kwa viongozi wa Serikali, taasisi za dini, jamii na vyombo vya habari kushirikiana kikamilifu katika kutoa elimu ya lishe bora kwa wananchi, ili kusaidia kuimarisha afya na maendeleo ya watoto na vijana.
Akizungumza na Mwananchi leo Septemba 19,2025 katika kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mkataba wa lishe kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa (RDC), Nyerere ameeleza kuwa lishe duni bado ni changamoto kubwa inayoathiri ukuaji wa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.
Amesema hali hiyo inayochangia udumavu na matatizo ya kiafya kwa watoto katika Mkoa wa Rukwa na taifa kwa ujumla.
“Ni wajibu wa kila kiongozi kutumia kila jukwaa analopata kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa lishe bora. Nawaomba viongozi wa dini wasaidie kufikisha ujumbe huu katika nyumba za ibada, wataalamu waendelee kutoa miongozo sahihi ya lishe, na vyombo vya habari viendelee kuelimisha jamii kupitia vipindi na makala,”amesema Nyerere
Licha ya Mkoa wa Rukwa kupata wastani wa asilimia 85 katika tathmini ya kitaifa ya utekelezaji wa afua za lishe, Nyerere amebainisha kuwa bado kuna changamoto ya kutotengwa kwa rasilimali fedha za kutosha katika halmashauri za mkoa wa Rukwa kwa ajili ya kutekeleza afua hizo muhimu kama ilivyokubaliwa kwenye Mkataba wa Lishe.
Aidha,amewataka wajumbe wa kikao hicho kuhakikisha kuwa mipango na bajeti za lishe zinawekewa vipaumbele katika mwaka wa fedha unaofuata, huku akisisitiza kuwa taifa lenye viwango vya juu vya udumavu haliwezi kufikia maendeleo endelevu.
“Tusimame pamoja kama Mkoa kuhakikisha kuwa tunawekeza ipasavyo katika lishe, kwa sababu taifa lenye watoto na vijana wenye udumavu ni taifa lenye changamoto katika nguvu kazi, elimu na uchumi. Ushirikiano wetu ndio msingi wa mabadiliko ya kweli,”amesisitiza Mkuu huyo wa Mkoa.
Nao baadhi ya washiriki kutoka taasisi ya Vipamaru ikiwakilishwa na Paul Sikaluzwe amesema endapo serikali itasimamia vizuri afua za lishe itasaidia kuondoa tatizo la udumavu.
Kikao hicho kimehudhuriwa na wakuu wa idara, wawakilishi wa halmashauri zote za mkoa wa Rukwa, wawakilishi wa taasisi zisizo za kiserikali,viongozi wa dini na wadau mbalimbali wa sekta ya lishe.