Mgombea udiwani wa Kata ya Vingunguti kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ndugu Omary Kumbilamoto, leo ameendelea na kampeni zake kwa kufanya mkutano wa hadhara katika Mtaa wa Kombo.
Katika mkutano huo, Kumbilamoto alinadi sera na Ilani ya CCM huku akieleza sababu zinazopaswa kuwashawishi wananchi wa Vingunguti kuichagua CCM kuanzia ngazi ya Urais, Ubunge hadi Udiwani.
Alisema kuwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, mgombea urais kwa tiketi ya CCM, ameonyesha uongozi makini kwa kutatua kero za wananchi hususan ujenzi wa madarasa, uboreshaji wa barabara na upatikanaji wa huduma za afya.
“Kwa kazi kubwa alizozifanya, hakuna kitu anachostahili Mama Samia zaidi ya kura za kishindo kutoka kwa wananchi wa Vingunguti na Tanzania kwa ujumla,” alisema Kumbilamoto.
Aidha, alitoa wito kwa wakazi wa Vingunguti kumchagua Mbunge Bonnah Kamoli, yeye mwenyewe kama diwani, na kumpa kura ya ushindi wa kishindo Mama Samia Suluhu Hassan katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.