Na Sophia Kingimali.
Waziri mkuu Kassim Majaliwa amesema elimu haiwezi kukamilika kama hakuna maadili kwani ndio yanayojenga utu,heshima na mshikamano katika jamii.
Hayo ameyasema jijini Dar es salaam Septemba 20,2025 alipomuwakilisha Rais Dk Samia Suluhu Hassan katika Hafla ya usiku wa utoaji tuzo za elimu za mufti.
Amesema Serikali inatambua mchango wa madhehebu ya dini ikiwemo BAKWATA na wadau wengine wa elimu katika kuimarisha maadili,kuendeleza maarifa na kuleta mshikamano wa kitaifa kupitia elimu.
“Serikali ya awamu ya sita imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha elimu inayotolewa nchini inakuza maarifa na ujuzi sambamba na malezi yanayoimarisha tabia bora na maadili ya kizalendo kwa kijana wa Kitanzania”,Amesema.
Akizungumzia tuzo hizo za Mufti amesema zinatambua ubunifu,uongozi,mshikamano wa jamii na mchango wa wadau katika kuhakikisha elimu inakuwa jumuishi,bora na endelevu.
“Tuzo za elimu za Mufti ni jukwaa la kitaifa la kutambua na kuthamani mchango wa kipekee katika elimu,ubunifu,malezi na maadili ya vijana wa Kitanzania lakini pia tukio hili linaakisi muonekano wa taifa lenye watu wanaojituma,wanaothamini elimu na wanaochangia ustawi wa Taifa letu bila kukali itikadi za dini au misimamo ya kisiasa”,amesema Majaliwa.
Aidha Majaliwa ameongeza kuwa Baraza Kuu la Kiislam BAKWATA limekuwa na mchango mkubwa katika kukuza sekta ya elimu nchini kwani limeazisha na kuendesha shule,madrasa na vyuo vinavyotoa elimu bora ya dini na kawaida,sambamba na kujenga maadili mema kwa vijana.
Kwa upande wake Mufti na Shekhe Mkuu wa Tanzania Abubakar Zuber amesema baraza hilo limekuwa likishughulika na elimu kwa muda mrefu na kipindi hiki wamekuja kushughulika zaidi ili kuhakikisha elimu nchini inazidi kuwa bora.
Amesema Bakwata imetoa mchango mkubwa sana kwenye elimu kwani imetoa viongozi mbalimbali katika nchi ambao wamesoma katika shule ambazo zipo chini ya baraza hilo zikiwemo Muslim,alhalamain,kibuhehe Jamuhuri na nyingine ambazo zipo chini ya BAKWATA
“Kuna watu leo ni mawaziri,wafanyabiashara wakubwa,kuna watu ambao ni wanasheria na watu aina mbalimbali ambao wamepita katika shule zetu ipo siku nitawataja kwa majina ili watu wajue mchango wa BAKWATA katika elimu”Amesema Mufti.
Nae,Mkurugenzi wa elimu BAKWATA Mwalimu Ally Abdallah amesema kupitia kauli mbiu ya mufti ya jitambue,badilika acha mazoea imeweza kufanikisha uwepo wa tuzo hizo
“Leo hii Mufti akiwa anatimiza miaka 10 ya utumishi wake uliotukuka anasheherekea kwa kutambua mchango wa wadau katika elimu kupitia tuzo ya elimu ya Mufti tuzo aliyoiasisi yeye mwenyewe tunamshukuru Mungu kwa kutupatia kiongozi huyu mwenye maono makubwa kwa nchi yake”,Amesema.
Aidha amesema kuwa Tuzo ya elimu ya mufti ni mpango ulibuniwa na mufti ili kusheherekea ubora wa taaluma kutambua na kukuza mbinu bora katika sekta ya elimu Tanzania
“Tuzo Hii ni kuwatia moyo wadau wa elimu wanaojitoa ipasavyo katika mabadiko chanya kwa maendeleo endelevu ya Taifa letu”Amesema.