DAR ES SALAAM, MCHEZAJI wa Karate Ramadhani Nassoro amechaguliwa kuiwakilisha Tanzania katika Mashindano ya Dunia ya Karate yatakayofanyika nchini Hungary mwezi Novemba mwaka huu.
Nassoro alipata nafasi hiyo baada ya Kamati ya Ufundi ya Shirikisho la Karate Tanzania (TSKF) kumteua kufuatia mafunzo ya kitaifa kwa wachezaji na waamuzi, yaliyohitimishwa Septemba 20, 2025 katika Klabu ya Upanga jijini Dar es Salaam.
Tanzania tayari imepokea mualiko rasmi kushiriki kwenye mashindano hayo, hatua inayotajwa kuongeza heshima kwa mchezo wa Karate nchini.
Katika mafunzo hayo, aliyekuwa Bingwa wa Karate barani Ulaya, Shihan Ali Tarabeih, ndiye aliyewaongoza wachezaji na waamuzi wa Tanzania. Bingwa huyo alisema atachagua wachezaji wawili na kuwapatia mafunzo maalumu ya kuongeza uwezo wao kwa viwango vya kimataifa.
Rais wa Shirikisho la Karate Tanzania, Yahaya Mgeni, alisema ujio wa bingwa huyo pamoja na uteuzi wa Nassoro kwenda Hungary ni dalili njema kwa mustakabali wa mchezo huo nchini.
“Tunataka Karate ya Tanzania iwe na jeuri ya kushindana nje ya mipaka, na hatua hizi ndizo zinafungua milango hiyo,” alisema Mgeni.
The post Nassoro kupeperusha bendera ya Tanzania Ulaya first appeared on SpotiLEO.