TANGA, TIMU ya ngumi ya Ngome inayomilikiwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) imetwaa ubingwa katika mashindano la Klabu Bingwa Taifa yaliyofanyika mkoani Tanga baada ya kuibuka na medali sita za dhahabu dhidi ya nne za MMJKT.
Ni baada ya miaka mitano bila ubingwa huo toka walipoutwaa kwa mara ya mwisho katika mashindano ya Iringa 2019 na kuupoteza kwa Tanzanite Manyara katika mashindano ya Manyara 2020.
Jumla ya klabu tisa kati ya 15 zilifanikiwa kupata medali katika mashindano hayo na zawadi za vikombe zikitolewa kwa wachezaji bora na anayechipukia, mwalimu bora, mwamuzi na jaji bora na timu yenye nidhamu.
Mchezaji bora wa kiume alichukua Faki Issa kutoka timu ya Jeba Boxing ya Tanga na kwa wanawake ilichukuliwa na Zainabu Kutaka kutoka MMJKT huku mchezaji anayechipukia ikichukuliwa na Issa Shabani kutoka Ngamiani ya Tanga.
Mwalimu bora wa mashindano hayo ilichukuliwa na Mzonge Mraba kutoka Ngome wakati Mwamuzi na Jaji bora ikichukuliwa na Saidi Hofu.
Timu yenye nidhamu bora ilichukuliwa na timu ya Magereza waliorudi vizuri kwenye ramani ya mchezo wa ngumi nchini, chini ya mwalimu wao Athony Kameda.
Moja ya mapambano ya fainali ya kuvutia yalikua kati ya mchezaji bora wa mashindano Faki Issa kutoka Jeba Boxing alipoweza kumsimamisha Maope Joseph kutoka MMJKT katika raundi ya pili katika uzani wa featherweight kg 57 huku Saidi Mtibala (Ngome) akishinda kwa pointi 3-2 dhidi ya Iddi Athumani kutoka MMJKT.
Mtambo mpya wa medali na mrithi wa Yusuf Changalawe kwenye uzani wa Light heavyweight kg 80, Bondia wa viwango Alphonce Abel kutoka MMJKT alifanikiwa kuibuka na ushindi wa KO raundi ya pili dhidi ya Milumbe James kutoka Ngome.
Kwa upande wa wanawake uzani wa light flyweight kg 50 Asha Iddi “Shisha” aliibuka kwa ushindi wa pointi 3-2 dhidi Marther Patrick wa Ngome aliyempa upinzani mkali huku katika uzani wa bantamweight kg 54 Zainabu Kutaka wa MMJKT akishinda kwa pointi 5-0 dhidi ya Vumilia Twalibu wa Ngome.
The post Ngome yatwaa ubingwa wa ngumi taifa first appeared on SpotiLEO.