DAR ES SALAAM: WIZARA ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imezitaka timu za mpira wa miguu zilizoomba kutumia Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa mashindano mbalimbali kuzingatia taratibu za matumizi ya uwanja huo.
Kauli hiyo imekuja kufuatia taarifa inayosambaa mitandaoni ikionesha wachezaji wa timu ya Pamba Jiji FC wakifanya mazoezi gizani katika Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es salaam jana.
Kwa mujibu wa taarifa iliyosainiwa na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Hassan Mabuye, timu zinapaswa kutoa taarifa mapema zinapotaka kufanya mazoezi ya mwisho kabla ya mechi ili maandalizi muhimu yafanyike badala ya kwenda ghafla na kusababisha sintofahamu isiyo ya lazima.
“Wizara imesikitishwa na usambazaji wa picha jongevu hiyo inayoonesha wachezaji wakifanya mazoezi gizani licha ya kuwa chanzo ni makosa ya timu ya Pamba Jiji FC yenyewe na imekiona kitendo hicho kama ni kuharibu heshima na taswira ya menejimenti ya uwanja ambayo imekuwa ikifanya kazi kuzingatia taratibu zilizowekwa,”ilisema taarifa.
Taarifa hiyo ilifafanua kuwa timu ya Pamba Jiji ilifika katika uwanja huo bila taarifa rasmi ya kwenda kufanya mazoezi ya kujiandaa na mchezo wao dhidi ya timu ya Yanga.
“Kwa kuwa timu haikuwa imetoa taarifa mapema, baada ya kuwasili katika uwanja huo majira ya saa 12.35 jioni wataalamu wa umeme uwanjani hapo walikuwa wameshaondoka, hivyo ikalazimu kuwarudisha kazini na kufanikiwa kuwasha taa za uwanja huo saa 1.08 usiku” ilisema taarifa hiyo.
The post Sakata la Pamba Jiji: Wizara yazitaka timu kufuata taratibu first appeared on SpotiLEO.