STAFFORDSHIRE: BAADA ya Kiungo mshambuliaji mpya wa Arsenal Eberechi Eze kufunga bao lake la kwanza ndani ya kikosi hicho katika ushindi wao wa mabao 2-0 wa Kombe la Carabao dhidi ya Port Vale usiku wa Jumatano, meneja wake Mikel Arteta anasema mchezaji huyo atakuwa na nyakati nzuri zaidi atakapopata muunganiko wachezaji wenzake.
Eze, aliyesajiliwa kutoka Crystal Palace kwa kitita cha pauni milioni 68 mwezi uliopita, alifungua akaunti ya mabao dhidi ya timu hiyo ya daraja la tatu katika dakika ya nane kabla ya Leandro Trossard kumaliza mchezo kwa bao la dakika ya 86.
Arteta amesema Eze alikuwa na utulivu wa hali ya juu katika kumiliki mpira dhidi ya timu iliyojipanga vyema kiulinzi na inayojua kudhibiti eneo lao la mwisho.
“Eze alicheza kwa utulivu mkubwa eneo la kati dhidi ya timu ambayo ni wazi ilicheza kwa mfumo 5-4-1, walibana sana waliziba mianya yote ya mipira yetu, tulikosa njia, si rahisi kupata nafasi lakini uwezo wake mkubwa wa kucheza mpira umetusaidia”
“Bado anahitaji muda zaidi wa kusoma alama za nyakati, haswa mambo ambayo anahitaji kufanya akiwa hapa. Halafu vitendo kama hivyo vitakuwa thabiti zaidi na bora kwetu. Kwa ujumla, ni mzuri sana bado kuna mengi zaidi ya kutupatia” – Arteta aliwaambia wanahabari baada ya mchezo huo.
Arsenal, ambao watawakaribisha Brighton katika raundi inayofuata ya Carabao Cup, watakuwa waheni wa Newcastle United katika mechi ya Ligi Kuu ya England Jumapili.
The post “Eze atafanya makubwa Arsenal” – Arteta first appeared on SpotiLEO.