FORT LAUDERDALE: KIUNGO wa zamani wa Barcelona na Hispania, Sergio Busquets, ametangaza rasmi kustaafu soka mwishoni mwa msimu wake wa sasa na Inter Miami klabu inayoshiriki ligi kuu ya Marekani Major League Soccer.
Busquets, mwenye miaka 37, anatajwa kama mmoja wa viungo wa ulinzi bora wa kizazi chake, akiwa sehemu ya utatu wa kihistoria wa Barcelona pamoja na Xavi Hernández na Andres Iniesta nyuma ya Lionel Messi.
Busquets alianza kucheza Barcelona mwaka 2008 chini ya kocha Pep Guardiola na alicheza mechi 722 kwa klabu hiyo kumweka katika nafasi ya tatu ya wachezaji waliocheza mechi nyingi zaidi nyuma ya Xavi na Messi huku akishinda mataji tisa ya ligi ya LaLiga na Ligi ya Mabingwa Ulaya mara tatu.
Yaliyokosekana kwake kwa kasi na kufunga mabao, lakini uwezo wake wa kupiga pasi sahihi, kuondoa mpira kwa usahihi na kuleta uwiano katika timu kwenye safu za ulinzi na mashambulizi. Hadi kupelekea Barcelona kumuita jiwe la msingi la Barcelona bora zaidi ya muda wote.
Busquets alicheza mechi 143 katika kikosi cha timu ya taifa ya Hispania, akishinda Kombe la Dunia mwaka 2010 na Ubingwa wa Ulaya mwaka 2012. Alikuwa nahodha wa Hispania alipostaafu timu ya taifa mwaka 2022.
Mwaka 2023, Busquets alijiunga na Inter Miami, akikutana tena na Messi pamoja na wachezaji wengine wa zamani wa Barcelona, Luis Suárez na Jordi Alba. Klabu hiyo imesema Busquets amekuwa mtu wa kazi maalum na ni moja ya viungo bora zaidi katika historia ya soka.
The post Busquets akubali yaishe, atangaza kustaafu soka first appeared on SpotiLEO.