A. MWANDISHI WETU – DAR ES SALAAM
KATIBU Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi amewataka wadau kushirikiana na Serikali katika kuimarisha hali ya lishe nchini ili kupunguza kasi ya kuenea kwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
Amesema ulaji usio faa na mitindo mibaya ya maisha vimechangia kuongezeka kwa magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza jambo linalohatarisha maendeleo ya Taifa.
Dkt. Yonazi ameyasema hayo jijini Dar es salaam leo 29 Septemba, 2025 katika Mkutano Mkuu wa 11 wa Wadau wa Lishe unaoendelea katika kituo cha mikutano cha APC Bunju.
Dkt. Yonazi amesema tafiti zinaonesha kuwa uzito uliozidi na uliokithiri ni chanzo kikuu cha magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza yakiwemo kisukari, moyo, figo na baadhi ya saratani.
“Napenda kukumbusha wadau, taasisi na wataalam kushirikiana na serikali kufanya tafiti zitakazosaidia kuleta majibu ya changamoto za lishe, pamoja na kusaidia watu kubadili tabia za ulaji na mtindo wa maisha ili kuzuia magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza yanayohusiana na ulaji usiofaa na ambayo ni tishio kwa Taifa letu,”alisema Dkt. Yonazi
Dkt.Yonazi ameongeza kuwa Takwimu zinaonesha licha ya hali ya lishe nchini kuendelea kuimarika bado kuna changamoto hususani kwenye uzito uliozidi na kiriba tumbo hii kutokana maendeleo tunayoyapata na mabadiliko ya mtindo wa maisha hususani ulaji usiofaa hivyo jitihada za pamoja kati ya wadau na serikali zinahitajika ili kukabiliana na tatizo hili.
Akizungumza kuhusu mkutano huo Dkt. Yonazi amesema lengo ni kupokea na kujadili hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa afua za lishe kwa kipindi cha Mwaka wa Tatu 2024/2025 katika maeneo mahsusi yaliyoanishwa kwenye Mpango Jumuishi wa Kitaifa wa Lishe (2021/22-2025/26).
Vilevile amesema mkutano huo unatoa fursa kwa wadau wote wa lishe kujadili namna utekelezaji ulivyofanyika, changamoto na mikakati ya kufanikisha utekelezaji katika kipindi kilichobaki cha utekelezaji wa mpango huo hususan mwaka 2025/26.
Kwa mujibu wa Dkt. Yonazi mkutano huo unatazamiwa kuongeza msukumo mpya wa utekelezaji wa afua za lishe miongoni mwa wadau kama moja ya nguzo muhimu kwa maendeleo ya Taifa.
“Uwepo wenu hapa, ni uthibitisho tosha wa ushirikiano mlionao na utayari wenu katika kuhamasisha uboreshaji wa hali ya lishe kwa Watanzania, hususani makundi yanayoathirika zaidi ambayo ni watoto wadogo na wachanga, watu wenye mahitaji maalum, wanawake wajawazito na wale walio katika umri wa uzazi,”amesema Dkt. Yonazi.
Dkt. Yonazi amewashukuru wadau wote walitoa mchango wa fedha na ushauri wa kitaalamu katika kufanikisha maandalizi ya mkutano huo na amewahakikishia kuwa serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za wadau ili kuhakikisha Taifa linapata mafanikio dhidi ya mapambano ya tatizo la utapiamlo.