Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) imetoa adhabu kwa Chama cha Soka cha Afrika Kusini (SAFA) baada ya kubainika kumchezesha Teboho Mokoena, mchezaji asiye na sifa za kushiriki, katika mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Lesotho uliochezwa mwezi Machi mwaka huu.
Kwa mujibu wa uamuzi huo, Afrika Kusini imenyang’anywa ushindi wake na sasa itaorodheshwa kupoteza mchezo huo kwa mabao 3-0. Aidha, SAFA imelazimika kulipa faini ya CHF 10,000 (takribani shilingi milioni 29 za Kitanzania) kwa FIFA.
FIFA imeipa SAFA siku 10 kuanzia tarehe ya kutolewa kwa uamuzi huu ili kukata rufaa endapo itaridhika kwamba uamuzi huo si sahihi.