DAR ES SALAAM:MSANII nyota wa muziki wa Bongo Fleva, Faustina Charles Mfinanga maarufu kama Nandy, ametoa kauli kali kufuatia hatua ya msanii mchanga kutoka Tanzania kudai kuwa wimbo wake mpya umefanana sana na kazi yake.
Inadaiwa kuwa msanii huyo chipukizi aliwasilisha malalamiko kwa YouTube, akiomba wimbo wa Nandy ushushwe (ufutwe) ndani ya siku sita kwa madai ya ukiukaji wa hakimiliki, akisema Nandy ameiga kazi yake inayojulikana kama “Joro”. Nandy hakukaa kimya.
Kupitia ukurasa wake wa mitandao ya kijamii, ameandika ujumbe mrefu akimueleza msanii huyo kuwa mafanikio hayaji kwa kuchafua kazi ya mwingine. Nandy alisema:
“Mdogo wangu, kutaka kuwa mkubwa kunahitaji juhudi. Kutaka kufika tulipo kunahitaji uwekezaji mkubwa sana… Ukiona mtu amefanikiwa, ujue kuna damu, jasho na machozi. Si kwa njia ya kuharibu kazi za wengine. Najua unajitafuta, lakini ulipofikia sasa ni sawa na kuua ndoto yangu…”
Nandy aliendelea kusisitiza kuwa msanii huyo hakupaswa kufungua madai ya hakimiliki kama njia ya kupata kiki au umaarufu, bali wangeweza kukutana na kuzungumza kama wasanii:
“Sitaki wasumbue IT wangu. Wewe na waliokushauri kutaka kushusha video yangu, mnaweza toa hiyo strike yenu. Sababu niamini, mdogo wangu, hiyo video ikishuka ukazika hela yangu chini, hata mama yako mzazi sitapokea msamaha wake.”
Kauli hii ya Nandy imeibua hisia tofauti mitandaoni, wengi wakijiuliza kama ni sahihi kwa msanii mkubwa kutoa majibu ya namna hiyo hadharani, badala ya kufikia suluhu kwa njia ya mazungumzo.
Mdau wa muziki Erick John alisema Nandy alikuwa na haki ya kulinda kazi yake na uwekezaji wake, hasa kama anaamini hajafanya kosa. Kazi ya sanaa huambatana na gharama kubwa na matarajio makubwa.
Hata hivyo, namna ya kujibu ina umuhimu mkubwa. Maneno ya Nandy, ingawa yanaeleweka kwa muktadha wa hasira na msongo wa mawazo, yameonekana kama ya kumdhalilisha msanii huyo mchanga hadharani.
Naye Shakira Juma alisema njia bora ingekuwa kukaa mezani na kuzungumza, hasa kama nia ya msanii mchanga haikuwa ya kutafuta kiki bali alihisi kudhulumiwa.
Pia kuna umuhimu wa wasanii chipukizi kujifunza njia sahihi za kudai haki bila kuharibu jina la mtu mwingine au kutumia njia za mkato kutafuta umaarufu.
The post Nandy apasua jipu kwa msanii chipukizi first appeared on SpotiLEO.